Serikali inajizatiti kuhakikisha Bandari ya Mombasa inakuwa na ushindani wa Kimataifa,kwa kuiwezesha kuboresha utendakazi wake.
Mwenyekiti wa kamati tekelezi ya kitaifa Dkt. Karanja Kibicho, amesema bandari hiyo ya Mombasa, itaendelea kutoa huduma za kuhakisha kuna maendeleo hapa nchini, huku akiwataka washikadau wote kushirikiana.
Kibicho, ambaye pia ni katibu katika wizara ya usalama alikuwa akiongoza ziara ya makatibu kumi wa wizara mbali mbali, kukagua miradi ya maendeleo katika eneo la pwani.

Aliwataka washikadau kuhakikisha bandari hiyo inavutia, na kuweza kushughulikia mizigo ya wale wanouza nje bidhaa, pamoja na wale wanoagia bidhaa kutoka nje ya nchi.
Alisema kuna haja ya kushughulikia tatizo la kucheleweshwa kwa mizigo ambalo linaathiri utendajikazi.
Dkt. Kibicho alisema, “Hatujazuru Bandari ya Mombasa kwa sababu kuna tatizo, ama kuna changamoto za utekelezaji Miradi ya maendeleo. Miradi hii ni muhimu sana katika kubadilisha uchumi wa taifa hili,”.

Serikali imeanza shughuli ya kupanua bandari hiyo kwa kuanzisha awamu ya pili ya ujenzi wa eneo la kupakia shehena, utakaogharibu shilingi bilioni 32.