Martha Wangari Karua ndiye mgombea mwenza wa muwaniaji Urais wa muungano wa Azimio la Umoja, One Kenya Raila Odinga katika uchaguzi mkuu wa tarehe tisa mwezi Agosti mwaka 2022.
Akimteua kuwa mgombea mwenza wake katika jumba la mikutano ya kimataifa jijini Nairobi, KICC, Raila alisema Karua ana tajiriba ya kutosha kuwa mgombea mwenza wake, na kwamba watashirikiana sako kwa bako kutimiza wajibu wao watakapotwaa uongozi wa taifa hili katika uchaguzi mkuu ujao.
Kutajwa kwa Karua kunajiri siku moja baada ya muungano wa Kenya kwanza kumteua mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua kuwa mgombea mwenza wake.
Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya ulibuni jopo la kuwasaili waliomezea mate wadhifa huo, wakiwemo, Gideon Moi, Martha Karua, Sabina Chege, Kalonzo Musyoka, Hassan Joho na Lee Kinyanjui, miongoni mwa wengine.