Jopo la Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) imemteua Jaji Martha Koome kuwa Jaji Mkuu mpya wa Kenya.
Kwenye kikao na waandishi wa habari leo alasiri, Profesa Olive Mugenda, ambaye ndiye anayeongoza jopo hilo, ametangaza kuwa Jaji Koome ndiye aliyeibuka kidedea kufuatia mahojiano ya wagombea yaliyotamatika wiki iliyopita.
Tangazo hilo limejiri saa chache tu baada ya Mahakama ya Rufaa kubatilisha agizo lililotolewa na Mahakama Kuu la kuzuia JSC kuendelea na usajili wa Jaji Mkuu wa Kenya.
JSC ilimsaili Jaji Koome pamoja na wagombea wengine wakiwemo Jaji Chitembwe Juma, Profesa Patricia Kameri Mbote, Jaji Marete Njagi, Wakili Philip Murgor, Jaji Nduma Mathews Nderi, Wakili Fred Ngatia, Jaji Ouko William Okello, Profesa Dkt. Dkt. Wekesa Moni na Wakili Alice Jepkoech Yano.
Kulingana na Profesa Mugenda, jina la Martha Koome tayari limewasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta kwa ajili ya uteuzi rasmi ikiwa Bunge litamuafiki.
Jaji Martha Koome, wa Mahakama ya Rufaa, atakuwa Jaji Mkuu wa kwanza mwanamke katika historia ya nchi hii.
Aidha, atakuwa wa 15 humu nchini na wa tatu chini ya katiba mpya na atachukua hatamu kutoka kwa David Maraga aliyestaafu kutoka kwa wadhifa huo.