Robert Matano wa Tusker Fc ndiye kocha bora katika ligi kuu ya Kenya mwezi wa Juni mwaka huu.
Matano ametawazwa mshindi baaada ya kuisaidia Tusker kushinda mechi 4 za mwezi Juni zilizowawezesha kuongoza jedwali la ligi kuu na kuwahi tiketi ya kushiriki ligi ya mabingwa barani Afrika.
Tusker walifungua mwezi kwa kushindwa bao 1-0 na Posta Rangers katika uwanja wa Ruaraka kabla ya kuilaza Kariobangi Sharks 1-0 uwanjani Utalii na kuwalemea Western Stima 2-1 katika uga wa Ruaraka na hatimaye kusajili ushindi wa magoli 4-1 dhidi ya Ulinzi Stars katika uwanja wa ASK Grounds kaunti ya Nakuru.
Ili kupokea tuzo hiyo Matano amewashinda Zedekiah Otieno wa KCB na aliyekuwa kocha wa Nairobi City Stars Sanjin Alagic na kushinda tuzo hiyo inayoandamana na zawadi ya shilingi elfu 50.
Matano ndiye kocha wa 6 kunyakua tuzo hiyo msimu huu baada ya Francis Kimanzi, Andre Casa Mbungo, Stanley Okumbi, na Vaz Pinto waliibuka washindi miezi ya Disemba , Januari, Februari, Machi , na Mei mtawalia.