Waziri wa usalama wa kitaifa Dr Fred Matiang’i anasema mzozo unaoshuhudiwa katika kaunti ya Laikipia huenda umechochewa kisiasa.
Matiang’i amekariri kwamba mizozo kama hiyo imekuwa ikizuka wakati nchi hii inapokaribia uchaguzi mkuu.
Hata hivyo ameihakikishia nchi hii kwamba wakati huu,oparesheni ya kiusalama itaendelea katika kaunti hiyo kwa muda zaidi ili kuhakikisha kuna uthabiti katika sehemu hiyo.

Waziri pia amewataka maafisa wa usalama wawe macho ili kutambua ishara za mapema za kuvurugwa kwa utulivu humu nchini, wakati huu ambapo nchi hii inajiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
Dkt. Matiang’i ambaye alikuwa akiwahutubia makamishna wa kaunti na warakibu wa maeneo Alhamisi asubuhi katika taasisi ya mafunzo kwa wafanyakazi wa serikali la Lower Kabete pia aliwashauri wabadili mbinu za kukabiliana na mizozo miongoni mwa jamii kupitia kwa mashauriano.
Kulingana na Dkt. Matiang’i wakenya wamekomaa na wanaweza kutafuta suluhisho kwa aina yoyote ya mzozo kupitia mashauriano wala sio kupitia kwa makabiliano.