Mbosso atangaza ujio wa Albamu yake

Mwanamuziki wa Tanzania kwa jina Mbosso Khan ametangaza kwamba atazindua albamu yake ya kwanza tarehe 14 mwezi Februari mwaka huu wa 2021 ambayo ni siku ya wapendanao ulimwenguni.

Siku hiyo ya wapendanao inaonekana kuwa wakati mwafaka wa kuachilia kazi hiyo yake kwani inahusu mapenzi na inaitwa “Defination of Love”.

Akizungumza wakati wa mahojiano asubihi ya leo kwenye kituo cha Wasafi Fm, Mbosso alifichua kwamba kwa kipindi fulani, baada ya bendi yake ya Yamoto kusambaratika, alikosa mpango wa kuendeleza muziki binafsi na akawa amezamia mpira wa miguu.

Rich Mavoko ndiye alikwenda kumtafuta nyumbani akampata akifanya mazoezi ya mpira wa miguu kisha akamchukua wakafanye colabo. Hivyo ndiyo aliingia WCB mpaka sasa.

Alisajiliwa na kampuni ya wanamuziki ya Wasafi Classic Baby – WCB yake Diamond Platnumz mwezi Januari mwaka 2018 na tangu wakati huo amekuwa akifanya vizuri katika ulingo wa muziki.

Mwezi Septemba mwaka 2020, Mbosso kwa jina halisi Joseph Kilungi, alijipatia kazi yake ya kwanza ya kuwa balozi wa bidhaa za maziwa za kampuni ya Tanga Fresh mkataba ambao nia yake ilikuwa kuongeza mauzo ya bidhaa hizo.

Mkubwa wake Diamond Platnumz alionekana kumpongeza kwa hatua hiyo huku akimtia moyo aendelee na kazi yake ya muziki.

Wakati huo pia, Mbosso alikiri kuwa na tatizo la kutetemeka mikono ambalo anasema alizaliwa nalo lakini wengi walidhani kwamba lilitokana na utumizi wa mihadarati lakini baadaye walielewa.

Alielezea kwamba katika hospitali zote alizozuru kutafuta tiba, madaktari walimwambia kwamba tatizo hilo haliwezi kurekebishwa na kwamba ataishi nalo milele.

  

Latest posts

Gurdian Angel Asifia Mpenzi Wake

Marion Bosire

Kibao Kipya cha Ringtone na Rose Muhando

Marion Bosire

Mulamwah Akaribisha Mwanawe

Marion Bosire

Tovuti hii inatumia kuki kukuhudumia vyema. Tafadhali kubali kupokea. Kubali Fahamu Zaidi