Msanii Q Chief atoa ilani kwa Wasafi Media

Msanii wa Bongo Fleva Q Chief ameupa usimamizi wa Wasafi Media na Kampuni ya Tigo muda hadi mwisho wa siku hii leo ili apate maelezo kamili kuhusu sababu ya kuweka jina lake na picha yake kwenye bango la tamasha lao bila idhini yake.

Kupitia Instagram, Q Chief alisema kwamba hakuna yeyote aliwasiliana naye rasmi kutoka kwa kampuni hizo ili kumshirikisha kwenye tamasha hilo la Jumamosi tarehe 30 mwezi Januari mwaka 2021 almaarufu kama “Wasafi Tumewasha na Tigo”.

Anaendelea kuelezea kwamba mashabiki wake wengi wamekuwa wakimpigia simu kujua ni kwa nini hakuonekana kwenye tamasha hilo ilhali walikuwa wakimtarajia jambo ambalo anasema linaathiri kazi yake ya muziki.

Q Chief anasema amekuwa akijaribu kuwasiliana na usimamizi wa Wasafi Media bila mafanikio huku akiambiwa kwamba wahusika bado wana uchovu wa tamasha la jumamosi.

Hata hivyo wengi wa mashabiki wake kwenye Instagram, wanaonelea kwamba hakustahili kuweka ilani hiyo kwenye mitandao ya kijamii na kwa kufanya vile wanahisi anajitafutia umaarufu.

Hakuna jibu lolote limetolewa na Wasafi Media inayomilikiwa na Diamond Platnumz wala kampuni ya mawasiliano ya rununu ya Tigo kuhusu lalama za Q Chief.

  

Latest posts

Rihanna Sasa ni Billionaire!

Marion Bosire

Diamond amwombea mema Haji Manara

Marion Bosire

Bin Kalama kuzikwa Jumapili

Marion Bosire

Tovuti hii inatumia kuki kukuhudumia vyema. Tafadhali kubali kupokea. Kubali Fahamu Zaidi