Mshairi wa umri mdogo zaidi wa uapisho wa Rais Marekani

Mwanadada Amanda Gorman wa miaka 22 tu amezungumziwa sana na kupata umaarufu kwenye mitandao ya kijamii ulimwenguni kote kutokana na jukumu lake kwenye uapisho wa Rais Joe Biden nchini Marekani.

Amanda ndiye alichaguliwa na kamati ya kusimamia uapisho wa Rais wa 46 wa Marekani Joe Biden tarehe 20 mwezi Januari mwaka 2021. Shairi lake lenye mada “The Hill we Climb” yaani “Kilima tunachokwea” liligusa nyoyo za wote waliofuatilia uapisho wa Biden.

Ndani ya shairi hilo alifichua kwamba yeye ni mtoto wa mhamiaji mweusi nchini Marekani na alilelewa na mama tu ilhali amepata nafasi ya kukariria Rais shairi.

Aligusia pia haja ya umoja wa watu wote nchini Marekani na uhuru wa kuchagua ambao alisema unaweza kucheleweshwa lakini hauwezi kushindwa kabisa.

Also Read
Bush ampongeza Biden kwa ushindi wa kura za Urais Marekani

Sauti yake tamu na ufasaha wa matamshi vilivutia zaidi huku wengi wakimshangilia. Amini usiamini, Amanda alikuwa na tatizo la kuzungumza akiwa wa umri mdogo.

Hata hivyo alipenda sana kuandika na kusoma na mamake ambaye ni mwalimu aliendelea kumtia moyo na hatimaye akaweza kulishinda tatizo hilo la kushindwa kuzungumza.

Gorman ambaye alifuzu kutoka chuo kikuu cha Havard anaendesha shirika kwa jina “One pen One Page” ambalo linahimiza vijana kuandika mashairi na hata hadithi.

Baada ya sherehe hiyo ya uapisho wa Joe Biden na Kamala Harris, wafuasi wa Amanda kwenye mitandao ya kijamii walikuwa wameongezeka maradufu.

Also Read
Rais Kenyatta ampongeza Rais Mteule wa Marekani Joe Biden

Kupitia Twitter alitoa shukrani zake huku akitaja wote ambao wamemtia moyo katika safari yake kama vile aliyekuwa mtangazaji wa runinga Bi. Oprah Winfrey.

Baadhi ya Marais nchini Marekani hususan wanne, wameonekana kuupa ushairi nafasi pale ambapo wanachagua mshairi kwa ajili ya sherehe zao za uapisho. Katika Historia ya taifa hilo, washairi ambao wametumika kwa sababu hiyo ni sita tu na Bi Amanda ndiye wa sita.

Mwaka 1961 mshairi Robert Frost alikariri shairi lenye mada “The Gift Outright” kwenye uapisho wa Rais John F Kennedy. Maya Angelou akakariri “On the Pulse of Morning” mwaka 1993 kwenye uapisho wa kwanza wa Bill Clinton huku Miller Williams akikariri “Of History and of Hope” kwenye uapisho wa pili wa Clinton mwaka 1997.

Also Read
Sakata ya Wasafi?

Katika uapisho wa kwanza wa Rais Barack Obama mwaka 2009, mshairi alikuwa Elizabeth Alexander na shairi liliitwa “Praise Song for the day”. Richard Blanco alikariri shairi “One Today” kwenye uapisho wa pili wa Rais Obama mwaka 2013.

Na wa mwisho ni mshairi nyota wa sasa Amanda Gorman ambaye pia ameandikisha historia kwa kuwa wa umri mdogo kati ya washairi wa sherehe za uapisho wa rais nchini Marekani.

  

Latest posts

Yul Edochie Amsifu Babake

Marion Bosire

Aki Na Paw Paw Warejea

Marion Bosire

Harmonize Atoa Orodha Ya Nyimbo Za Albamu Mpya

Marion Bosire

Tovuti hii inatumia kuki kukuhudumia vyema. Tafadhali kubali kupokea. Kubali Fahamu Zaidi