Maafisa wa upelezi wa Jinai DCI wamemtia nguvuni mshukiwa mkuu wa mauji ya shabiki sugu wa kandanda saac Juma Onyango mwenye umri wa miaka 58, aliyekatwakatwa hadi kufa Jumatano usiku muda mfupi baada ya saa tatu usiku.
Kulingana na DCI, mshukiwa huyo Milton Namatsi mwenye umri wa miaka 27, alikamatwa nyumbani kwake Mumias baada ya uchunguzi wa awali kumhusisha na mauaji hayo.
Inaaminika kuwa Juma na familia yake walikuwa wamekula chakula chajioni nyumbani kwao katika kijiji cha Ebuyenjere, wakati shambulizi hilo lilipotokea.
Mapema usiku huo watoto waliokuwa wakila chakula chao nje ya Nyumba, walisema waliona watu wakiingia ndani ya noma kupitia ua.
”Waliripoti kisa hicho kwa wazazi wao lakini wazazi walipuuza. Muda mfupi baadaye walisikia mvurugano katika zizi la kondoo na kumlazimu Juma akiandamana na kijana wake wa umri wa miaka 17 kutoka nje,” DCI.
”lakini kabla ya kubaini kilichojiri, wavamizi hao walimshambulia Juma hadi akafariki. Mtoto wake hata hivyo alinusurika kifo kwa kutorokea shambani,” ilisema idara ya polisi.
Majajusi wanashuku kifo cha Juma kilitokana na mzozo wa ardhi, huku wakisema wanafanya kila wawezalo kuwatia mbaroni washukiwa hao wengine.
Isaac Juma ambaye alikuwa akiuza gazeti kabla ya kustaafu nyumbani kwake Mumias, amekuwa shabiki sugu wa timu ya taifa harambee stars na klabu ya AFC Leopards.
Mshukiwa huyo anazuiliwa katika korokoro za polisi akisubiri kufikishwa Mahakama kujibu mashtaka ya mauaji.