Mudavadi ajitosa rasmi ulingoni huku mwangwi wa BBI ukivuma kote nchini

Kiongozi wa chama cha Amani National Congress, ANC, Musalia Mudavadi ametangaza rasmi kuunga mkono ripoti ya BBI.

Kulingana na Mudavadi chama cha ANC kitaongoza shughuli ya ukusanyaji sahihi kote nchini na kuanzisha kampeni yake kupigia debe ripoti hiyo sambamba na ile inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

“Baada ya mashauriano na wanachama, chama cha ANC kitaunda mpango wake wa kuipigia debe ripoti hiyo,” ametangaza Mudavadi.

Mudavadi amesema ripoti ya mwisho ya BBI iliyozinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wiki iliyopita imefanyiwa marekebisho na inajumuisha matakwa ya Wakenya wote.

Also Read
Mahakama ya rufaa kutoa mwongozo kuhusu kesi za BBI wiki ijayo

“Chama cha ANC kinawahimiza Wakenya wote kushiriki katika mchakato huu kwa nia ya kuwa na kura ya maamuzi isiyo na upinzani,” ameongeza Mudavadi.

Hayo yanajiri huku Mbunge wa Ruiru Simon King’ara akiwahimiza wakazi wa Eneo Bunge lake kuweka sahihi fomu za BBI zinazosambazwa katika sehemu hiyo.

Hata hivyo mbunge huyo amefafanua kwamba kuweka sahihi kwenye fomu hizo hakumaanishi wanaunga mkono kura ya maamuzi, bali ni mwanzo wa shughuli ya marekebisho ya katiba.

Also Read
Raila awasili Pwani kupigia debe BBI lakini Joho, Kingi wakosa kumlaki

Akiongea katika wadi ya Gitothua katika eneo bunge lake ambako alitoa msaada wa mablanketi, magodoro na nguo kwa zaidi ya waathiriwa 20 wa moto ulioteketeza nyumba zao, King’ara amesema mchakato wa BBI ndio suluhisho la ugavi sawa wa raslimali za kitaifa.

“Kuweka saini si kusema umeamua, ni kusema umekubali mambo yaendelee na wakati wa kupiga kura utatoa uamuzi wako,” ameeleza King’ara.

Ruiru ni miongoni mwa maeneo bunge sita yaliyopendekezwa kugawanywa katika kaunti ya Kiambu iwapo katiba itafanyiwa marekebisho.

Naye Mwenyekiti wa chama cha Jubilee katika Kaunti ya Kirinyaga Mureithi Kang’ara amewahimiza wakazi wa kaunti hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la ukusanyaji saini za BBI.

Also Read
Mvua kubwa yawahofisha wakazi wa Pokot Magharibi

Akiongea mjini Kagio muda mfupi baada ya kuweka saini yake, Kangara amesifia mapendekezo ya ripoti hiyo iliyoorodhesha Kaunti ya Kirinyaga kuwa mojawapo ya kaunti zitakazonufaika na eneo bunge jipya.

Kang’ara amesema chama cha Jubilee kinafanya kazi kwa pamoja kwenye shughuli ya kukusanya saini za marekebisho ya katiba.

Shughuli ya kukusanya saini ilizinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.

  

Latest posts

Mwanafunzi ateketeza bweni kukwepa kufanya mitihani Tharaka Nithi

Tom Mathinji

Mahakama yamzuia Mohammed Badi kuhudhuria mikutano ya Baraza la Mawaziri

Tom Mathinji

IEBC yalenga kuwasajili wapiga kura wapya milioni sita kabla Uchaguzi Mkuu ujao

Tom Mathinji

Tovuti hii inatumia kuki kukuhudumia vyema. Tafadhali kubali kupokea. Kubali Fahamu Zaidi