Mwanafunzi wa zamani wa shule ya wasichana ya Moi jijini Nairobi aliyepatikana na hatia ya kuua bila kukusudia kutokana na mkasa wa moto wa mwaka 2017, uliosababisha vifo vya wanafunzi tisa amehukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani.
Akitoa uamuzi huo, jaji Stella Mutuku alisema aliafikia uamuzi huo kwa kufuata sheria na ushauri wa maafisa kutoka mahakama ya rufaa.
Aidha, jaji huyo alisema mshukiwa huyo hakuanzisha moto huo kwa lengo la kuwaua wanafunzi wenzake, lakini alikuwa akitumia mbinu zote ili ahamishwe kutoka shule hiyo.
Wakati wa mkasa huo wa moto, mwanafunzi huyo alikuwa na umri wa miaka 14.
Jaji Mutuku alisema wazazi waliopoteza mabinti zao kupitia moto huo wanakabiliwa na mahangaiko.
Hukumu hiyo itatekelezwa kuanzia wakati mtoto huyo alipopatikana na hatia mwezi Disemba mwaka 2021.
Kabla ya kisa hicho, ilisemekana mtoto huyo alijaribu kujiua zaidi ya mara mbili kabla ya kuamua kuchoma bweni la shule hiyo.
Imesemekana moto huo ulianzia chumba cha mshukiwa kabla ya kusambaa hadi vyumba vya karibu na kisha kuharibu bweni zima la zaidi ya wanafunzi 300.
Familia za waathiriwa hata hivyo zimetaja hukumu hiyo ya kifungo cha miaka mitano, kuwa nyepesi.