Mwanamme mmoja nchini Marekani ndiye binadamu wa kwanza kupachikwa moyo mbadala wa nguruwe kupitia mbinu ya kisayansi ya GMO.
Madaktari wamesema David Bennett mwenye umri wa miaka 57 anaendelea vyema siku tatu tangu upasuaji huo wa majaribio uliodumu kwa takribani saa 7 huko Baltimore.
Upasuaji huo wa kubadilisha moyo ulikuwa hatua ya mwisho ya kujaribu kuokoa maisha ya Bennett japo haijulikani ataisha na moyo huo mbadala kwa muda gani.
Madaktari kutoka kituo cha matibabu katika chuo kikuu cha Maryland walipata idhini maalum kutoka idara ya kudhibiti shughuli za kimatibabu na dawa nchini Marekani kufanya upasuaji huo ili kuokoa maisha ya mgojwa huyo.
Aidha iliaminika kuwa mgonjwa huyo hangestahimili upasuaji huo. Daktari wa tiba ya moyo Bartley Griffith, alisema upasuaji huo ni dhihirisho la uwezekano wa Ulimwengu kuafikia suluhu kwa tatizo la uhaba wa moyo kwa wanaohitaji upachikaji.