Naibu Gavana wa Kilifi Gideon Saburi atangaza kuwania ugavana 2022

Naibu Gavana wa Kaunti ya Kilifi Gideo Saburi ametangaza azma ya kutaka kumrithi mkuu wake Amason Kingi kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Saburi aliteuliwa na Gavana Kingi kama mgombea mwenza kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 baada ya aliyekuwa naibu gavana wakati huo Kenneth Kamto kuhitilafiana na Kingi.

Saburi na Kamto wanatoka katika jamii ya Rabai, hali ambayo wachanganuzi wa kisiasa wanasema Gavana Kingi alipendelea kimakusudi kuchagua mgombea mwenza kutoka jamii hiyo ili kutafuta uungwaji mkono zaidi katika eneo hilo.

Also Read
Wabunge waliokutana na Ruto wasema marekebisho ya katiba si kipaumbele kwa sasa

Akitangaza azma yake kwenye hafla ya mazishi ya Ruth Kombo, ambaye ni mamaye aliyekuwa Mwakilishi Wadi ya Ruruma Naftali Kombo, Saburi amesema kipindi alichohudumu kama naibu gavana kimempa tajriba ya kutosha ya kuendesha shughuli za kaunti ya Kilifi baada ya Kingi kustaafu mwaka ujao.

“Hapa Rabai tumekuwa na manaibu mara mbili, sasa naona tumeiva na tunataka tuingie katika nafasi ya ugavana,” akasema Saburi.

Also Read
Joho, Kingi waanzisha mchakato wa kuunganisha Pwani kabla uchaguzi mkuu wa 2022

Kauli hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Rabai William Kamoti pamoja na viongozi wengine wa eneo hilo ambao walihimiza umoja wa jamii hiyo ili kuafikia tamanio la jamii hiyo kurithi wadhifa huo.

Jina la Saburi liligonga vichwa vya habari mnamo mwezi Machi mwaka uliopita baada ya kushtumiwa na hata kufunguliwa mashtaka kwa madai ya kusambaza virusi vya korona kimakusudi katika eneo la Kilifi aliporejea kutoka ziara ya ng’ambo.

Wanasiasa wengine ambao wametangaza kuwania ugavana wa kaunti hiyo ni pamoja na Katibu Mwandamizi wa Wizara ya Ardhi Gideon Mung’aro, Seneta wa kaunti hiyo Stewart Madzayo, Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na mwenzake wa Magarini Michael Kingi, ambaye ni kakake Gavana Amason Kingi.

Also Read
Viongozi wa Pwani waahidi kuzindua chama cha Wapwani

Haijabainika kama aliyekuwa Mbunge wa Kaloleni Kazungu Kambi atajitosa tena kwenye kinyang’anyiro hicho, huku kukiwa na tetesi kwamba Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya amejitoa kinyang’anyironi hata baada ya kutangaza kuwania nafasi hiyo awali.

  

Latest posts

Rais Kenyatta amwomboleza Nancy Karoney, dadake waziri wa ardhi Farida Karoney

Tom Mathinji

Mutahi Kagwe: Wahudumu wa afya wafeli katika somo la Kingereza

Tom Mathinji

Prof Magoha: Awamu ya kwanza ya ujenzi wa madarasa ya CBC kukamilika mwezi Aprili mwakani

Tom Mathinji

Tovuti hii inatumia kuki kukuhudumia vyema. Tafadhali kubali kupokea. Kubali Fahamu Zaidi