Ripoti ya hivi punde ya makadirio ya maambukizi ya maradhi ya virusi vya ukimwi, inaonyesha kuwa Kaunti ya Nairobi kwa sasa ndiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi nchini.
Ripoti hiyo inakadiria kuwa wakazi 167,446 wa Nairobi wana virusi hivyo. Ripoti hiyo pia ilionyesha kuwa maambukizi mapya 4,446 yalitokea mnamo mwaka 2020, huku vijana wakichangia asilimia 33 ya maambukizi mapya.
Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri ya Utoaji Huduma katika maeneo ya jiji la Nairobi (NMS), Mohammed Badi, alisema katika taarifa kwamba wameweka mikakati kadhaa kukabiliana na hali hiyo.
Alisema wamejitolea kuangamiza ueneaji wa janga la ukimwi ifikapo mwaka 2030.
Badi alisema kuwa halmashauri hiyo imeanzindua hospitali mpya 24 zenye vitengo vya kuzuia na kudhibiti ueneaji wa ukimwi ili kuhamasisha upimaji wa virusi vya ukimwi hasa miongoni mwa vijana.
Alisema halmashauri hiyo pia inaimarisha uwezo wa kukabiliana na pengo la ujuzi wa kuwawezesha vijana kushughulikia maswala ya uzazi, na yale yanayohusiana na virusi vya ukimwi.