Wanamuziki wa Tanzania Nandy na Billnass wanaendelea kuandaa harusi yao ambayo inatarajiwa kufanyika mwezi wa sita mwaka huu wa 2022. Hii ni baada ya Billnass kumvisha Nandy pete ya uchumba ambayo anasemekana kupoteza kwenye tamasha moja la kampeni za kisiasa za chama cha CCM. Billnass alirudia kumvisha Nandy pete kwenye sherehe ya utambulisho nyumbani kwa wazazi wa Nandy na hapo ndipo walianza maandalizi ya kufunga ndoa.
Billnass ambaye jina lake halisi ni William Nicholaus Lyimo alichapisha video fupi ambayo inamwonyesha akijipima suti na kuandika maneno haya, “William kama William azimio letu ni lile lile maamuzi yanaweza kubadilika dakika yoyote ya mchezo hata nusu saa kabla ya kuingia kanisani.” Nandy alijibu kwa utani akisema kwamba tayari ametafuta mganga wa Nigeria ambaye ana uwezo wa kumgeuza akawa kunguni iwapo atabadili mawazo kuhusu kumwoa.
Wawili hao wamekuwa wapenzi kwa muda mrefu. Wakati mmoja waliachana, Nandy akaingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na marehemu Ruge Mutahaba ambaye aliaga dunia na baadaye tena akarudiana na Billnass. Kumekuwa na tetesi kwamba Nandy ni mjamzito jambo ambalo anakana. Mwaka 2019 alikiri kwamba aliwahi kubeba mimba ya Billnass lakini ikaharibika.
Wakati mmoja wawili hao walifungiana kwenye mitandao ya kijamii na kusababisha minong’ono kwamba wameachana lakini ikagundulika bado walikuwa pamoja.