Bukeni Ali mwanamuziki ambaye anajulikana sana kama Nubian Li ambaye ni mwendani wa karibu wa mwanamuziki aliyepia kiongozi wa chama cha National Unity Platform (NUP),Robert Kyagulanyi au ukipenda Bobi Wine amefunga ndoa.
Li alihalalisha ndoa kati yake na mpenzi wake wa muda mrefu Mutoni Salha katika msikiti wa Kibuli. Wawili hao wamekuwa pamoja kwa muda mrefu na wamebarikiwa na watoto watatu, wasichana wawili na mvulana mmoja.
Arusi yao ilihudhuriwa na watu wengi maarufu nchini Uganda akiwemo Bobi Wine, mke wake Barbie, mbunge wa Mityana Francis Zaake, kati ya wengine wengi.
Urafiki kati ya Nubian Li na Bobi Wine ni wa kipekee ambapo Nubian na wafuasi wengine wa Bobi Wine walitiwa mbaroni wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu nchini Uganda mwezi Disemba mwaka 2020 kwa madai ya kuandaa mikutano ya umma bila kujali na kutishia maisha ya wananchi kupitia kutengeneza mazingira ya kusambaa haraka kwa virusi vya korona.
Akizungumza kwenye hafla ya arusi ya Nubian na Mutoni, Bobi Wine alimsifia sana rafiki yake akisema amekuwa kama ndugu kwake. Alifichua kwamba Nubian ndiye alimsukuma aingilie siasa. Alimshukuru kwa kumchagua awe msimaizi wake kwenye arusi yake akisema hakuna mtu amewahi kumtunuku fursa kama hiyo ambayo anaichukulia kuwa ya kipekee.
Nubian Li na Bobi Wine walipata nafasi ya kumwimbia Mutoni Salha siku hiyo ya arusi.