Aliyekuwa Rais wa shirikisho la kandanda nchini FKF Sam Nyamweya ameishutumu afisi ya sasa kwa kuchangia matokeo mabaya ya timu ya taifa Harambee Stars .
Kwenye mahojiano Nyamweya ameikosoa afisi ya Nick Mwendwa na benchi ya kiufundi kwa kuwaacha nje wachezaji wenye tajriba kwa mechi mbili za mwanzo za kundi E ,kufuzu kwa fainali za kombe la dunia dhidi ya Uganda na Rwanda .
Kinara huyo wa zamani ameongeza kuwa mabadiliko katika kikosi yanapaswa kuwa ya taratibu na wala sio mara moja ili kuhakisha wachezaji chipukizi wanapata morali kutoka kwa wale wazoevu.
Kumekuwa na shutma kutokana na jinsi wachezaji Victor Wanyama wa Montreal Impact,Ayub Timbe na Johanna Omolo miongoni mwa wengine walivyochujwa kwenye kikosi na kocha Jacob Mulee kwa mechi za kundi E kufuzu kwa fainali za kombe la dunia mwaka ujao ,michuano iliyochezwa wiki jana.
Nyamweya pia anaamini kuwa Harambee Stars inahitaji mkufunzi wa kigeni ambaye atakuwa huru kuwateua wachezaji kikosini bila mapendeleo wala kushurutishwa.
Harambee Stars ambayo ni ya tatu kundini E kufuzu kwa fainali za kombe la dunia mwaka ujao,itazuru Yaounde Cameroon Oktoba 9 kumenyana na Mali kwa mchuano wa tatu .