Paul Kipkemoi Chelimo ambaye ni mshindi wa nishani ya fedha ya Olimpiki katika mita 5000 mwaka 2016 na shaba ya dunia katika shindano hilo mwaka 2017, ni mwanariadha aliyehamia nchini Marekani na kubadilisha uraia wake takriban miaka 10 iliyopita.
Chelimo aliye na umri wa miaka 31 na anayefanya kazi katika jeshi la Marekani ameshiriki mashindano humu nchini mara mbili mwaka huu,mwanzo katika mbio za Nyika za Agnes Tirop memorial cross country Februari 13 ,ingawa hakukamilisha shindano.
Pia mwanariadha huyo alishinda nishani ya shaba ya Olimpiki katika mita 5000 mwaka 2021.
Chelimo alishiriki makala ya 3 ya mashindano ya Kip Keino Classic continental tour katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani ,akitimka mbio za mita 1500 ili kutafuta kasi anapojiandaa kuwinda taji ya dunia ya mita 5,000 na mita 10,000 mjini Oregon Marekani.
Chelimo alimaliza katika nafasi ya 10 kwenye fainali hiyo iliyoshindwa na Mkenya Abel Kipsang.
Kwenye mahojiano baada ya kukamilisha shindano la Jumamosi iliyopita,Chelimo alisema ilikuwa ni fahari yake kurejea kushindana uwanjani Kasarani kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2013 na anaangazia kunyakua dhahabu ya dunia mwaka huu ,mashindano yatakayoandaliwa nchini Marekanikati ya Julai 15-24 mwaka huu.
Mwanariadha huyo ni mzawa wa Iten wazazi wake wakiwa Gabriel Suter na Roselyne Cheruiyot akiwa na kaka watatu , Moses Kiptoo, Denis Chelimo na Alberto Chelimo, na dada mmoja Emmanuela Chelimo.
Chelimo alipewa uraia wa Marekani mwaka 2014 baada ya kujiunga na jeshi la nchini na alingia nchini Marekani kupitia msaada wa masomo mwaka 2010 .