Wakenya sasa watakuwa wakipokea huduma za ardhi popote walipo kufuatia uzinduzi wa mfumo wa kidijitali wa habari kuhusu ardhi.
Akizindua mfumo huo maarufu kama ‘Ardhi Sasa’ leo alasiri, Rais Uhuru Kenyatta amesema huduma za ardhi sasa zitaendeshwa pasi na hofu ya ulaghai.
Mfumo huo mpya unatarajiwa kuimarisha usalama wa rekodi za ardhi, kuongeza kasi ya biashara za ardhi na pia kukomesha ulaghai katika maswala hayo.
Rais amesema Ardhisasa itasaidia pakubwa kubaini uhalali wa stakabadhi za ardhi kwa wauzaji na wanunuzi, hali ambayo imekuwa chanzo cha wasi wasi miongoni mwa wauzaji na wanunuzi wa ardhi nchini.
Aidha Rais ameusifu mfumo huo kwamba utakuwa chemichemi ya habari sahihi kusaidia Idara za Upelelezi wanaposhughulikia masuala ya ardhi.
Ametoa wito kwa wakenya kutumia mfumo huo wa kiwango cha kimataifa jijini Nairobi kubaini uhalalai wa hati miliki lzao.
Mfumo wa Ardhisasa ulitayarishwa na kundi la Wakenya katika muda wa miaka mitatu na ni mradi ulioanzishwa na serikali ya kitaifa kupitia kwa Rais Uhuru Kenyatta.
Mfumo huo wa kuweka shughuli za ardhi kwenye mtandao utazinduliwa kwa awamu katika sehemu nyingine nchini.