Rais Uhuru Kenyatta ametuma risala za rambirambi kwa serikali na raia wa muungano wa milki za Kiarabu, kufuatia kifo cha Rais Sheikh Khalifa bin Zayed Al Nahyan, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 73.
“Kwa niaba ya serikali na raia wa Kenya na pia kwa niaba yangu mwenyewe, natuma rambirambi kwa serikali na raia wa muungano wa milki za Kiarabu kufuatia kifo cha Rais Sheikh Khalifa bin Zayed Al Nahyan,” alisema Rais Kenyatta.
Rais Kenyatta alimuomboleza marehemu Sheikh Khalifa kuwa kiongozi aliyebadilisha taifa hilo la ghuba kuwa kitovu kikuu cha kiuchumi.
“Mawazo yetu na maombi yetu yako kwa familia, serikali na raia wa muungano wa milki za Kiarabu, wakati huu mgumu wa majonzi,” aliomboleza Rais Kenyatta.
Kiongozi wa taifa alisema Kenya inaiombea kwa Mola muungano wa milki za Kiarabu wakati huu unapoimboleza kifo cha kiongozi wake.