Rais Uhuru Kenyatta ametaka kuwekwa kwa mikakati ya kuhakikisha vijana wanaweza kunufaika na vipaji vyao hapa nchini.
Rais Kenyatta aliwapongeza vijana wa hapa nchini ambao hujitolea kutenda wema katika jamii zao kupitia kujitolea na kutia bidii.
Akiongea wakati wa utoaji tuzo za Rais kwa vijana wenye vipaji mbali mbali, kiongozi wa taifa alisema vijana ndio wanaoshikilia hatma ya taifa hili hivyo basi ni muhimu kuwazingatia.
“Katika shughuli zangu za kirais, shughuli ambazo huwa nazitazamia sana ni zile zinazowahusu vijana kwa kuwa wao ndio wanashikilia hatima ya taifa hili,” alisema kiongozi wa taifa.
Rais alisema vijana wote wana vipaji na kwamba ni jukumu lao kufahamu talanta zao.
Huku akimpongeza mwanariadha Ferdinand Omanyala kutokana na juhudi zake za kukimbia mbio za mita 100, Rais Kenyatta alitoa wito kwa vijana kuiga mfano wa Omanyala, kwani wana uwezo wa kupeleka taifa hili katika hatua nyingine.
Jumla ya vijana 907 wakitunzwa, miongoni mwao vijana 25 wanaoishi na ulemavu, waliopokea vyeti kutokana na matokeo ya kupigiwa mfano katika taasisi na jamii wanazotoka.