Rasimu ya kwanza kuhusu makubaliano ya jinsi ambavyo mataifa mbali mbali duniani yatapungzua kiwango cha uchafuzi wa hewa ili kuepusha uwezekano wa Joto kupanda hadi zaidi ya nyuzi 1.5 imechapishwa.
Uingereza ambayo ndiyo mwenyeji wa mkutano wa umoja wa mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa Jijini Glasgow ilichapisha siku ya Jumatano rasimu ya uamuzi huo wa kisiasa, ambao utajadiliwa katika muda wa siku chache zijazo, na kuhimiza mataifa ya dunia kuboresha mipango yao ya kitaifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa ifikapo mwisho wa mwaka 2022.
Rasimu hiyo inaangazia kile ambacho wajumbe wanatumai yatakuwa matokeo ya mkutano huo wa (COP26).
Inahimiza nchi tajiri kuongeza misaada yao kwa nchi masikini. Aidha, rasimu hiyo kwa mara ya kwanza inahimiza mataifa ya dunia kutamatisha utumizi wa makaa ya mawe na fidia nyinginezo kwa mafuta ya petroli.
Rasimu hiyo yenye kurasa Saba inaangazia kuidhinishwa kwake – na hivyo kuwezesha nchi za dunia kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani na pia ufadhili.
Wajumbe kutoka karibu nchi 200 zinazowakilishwe kwenye mkutano wa (COP26), watakutana Jumatano kujadili taarifa ya mwisho ambayo watakuwa tayari kutia saini wakati wa kumalizika kwa mkutano huo mwishoni mwa Juma hili.