Ligi kuu ya Kenya , KPL na ligi kuu ya daraja ya kwanza NSL zitarejelewa Jumamosi hii Disemba 4 ,baada ya kusitishwa kwa takriban mwezi mmoja kutokana na majukumu ya timu ya taifa Harambee Stars na baadae kuvunjiliwa mbali kwa shirikisho la soka Kenya FKF na waziri wa Michezo Dkt Amina Mohammed.
Kulingana na ratiba hiyo,Kariobangi Sharks itachuana na Nairobi City Stars Jumamosi katika uwanja wa Ruaraka saa saba Adhuhuri,wakati Bidco United Fc ikiwaalika AFC Leopards katika uwanja wa manispaa wa Thika pia saa saba.
Nzoia Sugar itakuwa nyumbani uwanja wa Sudi Bungoma kuanzia saa tisa, dhidi ya Kakamega Homeboyz nayo Ulinzi Stars FC iwatembelee Wazito FC katika uga wa kimataifa wa Kasarani pia saa tisa,.
Mathare United itakuwa na miadi dhidi ya Fc Talanta saa tisa uwanjani Kasarani kisha ,Kenya Police wafunge kazi dhidi ya Sofapaka uwanja wa Ruaraka saa tisa na robo.
Jumapili kutachezwa mchuano mmoja pekee KCB FC, ikikabana koo na Vihiga Bulltes FC katika uwanja wa Utalii,baada ya mechi za Gor Mahia dhidi ya Posta Rangers na ya Bandari FC na Tusker FC kuahirishwa kutokana na mechi za bara Afrika .