Rais wa Russia Vladimir Putin ameonya mwenzake wa Finland dhidi ya kujiunga na shirika la kujihami la NATO. Anasema kwamba hatua kama hiyo ni kosa kubwa na kwamba itasababisha kuvunjika kwa uhusiano mwema ulioko kati ya nchi hizo mbili. Putin alimwambia Sauli Niinisto kwamba hakuna tishio lolote dhidi ya usalam wa nchi ya Finland.
Viongozi hao wawili walizungumza kwa njia ya simu huku Finland ikijiandaa kutoa tangazo rasmi karibuni. Niniisto alimpigia Putin simu ili kumjuza kuhusu wazo hilo. Sweden pia imeonyesha nia ya kujiunga na shirika la NATO kufuatia hatua ya Russia ya kuvamia Ukraine. Finland ina mpaka wa kilomita 1300 na Russia na imesalia nje ya shirika la NATO hadi sasa ili kutokera jirani yake wa upande wa mashariki.
Putin hakutoa tishio lolote dhidi ya Finland kuhusu wazo la kujiunga na NATO lakini wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema kwamba watalipiza kisasi. Uamuzi wa Russia wa kukomesha mauzo ya bidhaa za kielekroniki kwenda Finland unachukuliwa kuwa ishara ya mwanzo ya kisasi.
Rais Niniisto anasema mazungumzo yao yalikuwa wazi bila utata. Anasema alifahamisha Putin kuhusu haja ya kila nchi kuchukulia kwa uzito usalama wake wakati walikutana kwa mara ya kwanza mwaka 2012 wakati alichaguliwa kuiongoza Finland.