Safari nyingi za ndege zimefutiliwa mbali nchini marekani katika msimu huu wa krismasi kutokana na athari za janga la Covid-19 na hali mbaya ya anga.
Takriban safari 4,400 za ndege zilifutiliwa mbali siku ya Jumamosi huku zaidi ya safari 2,500 zikifutiliwa mbali nchini Marekani.
Baadhi ya mashirika ya ndege yameathirika vibaya na janga la Covid-19 huku wafanyikazi wakiambukizwa virusi hivyo na kulazimika kwenda karantini.
Aidha kumekuwa na hali mbaya ya anga ya theluji katika eneo la kati mwa marekani. Inatarajiwa kuwa watu wengi wataathirika zaidi siku ya jumapili watakapokuwa wakijaribu kurejea kutoka likizo za krismasi.
Vyama vya wafanyikazi vinasema kuwa wafanyikazi wanaogopa kuambukizwa virusi vya corona au kukabiliana na abiria walio na gadhabu. Visa vya maambukizi ya virusi vya corona aina ya Omicron vinazidi kuongezeka nchini marekani.
Mji wa New York umenakili visa vingi licha ya kuchanja idadi kubwa ya wakazi wake.