Rais Uhuru Kenyatta amesema serikali Iko katika harakati za kujenga hospitali ya kiwango cha kimataifa ya kushughulikia afya ya akili, kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na changamoto za afya ya akili hapa nchini.
Akizungumza wakati wa mazungumzo na Kamel Ghribi ambaye ni mwenyekiti wa GKSD mojawepo ya hospitali kuu ya kibinafsi nchini Italia, Rais Kenyatta alisema afya ya akili ni changamoto inayoongezeka hapa nchini, na kutoa haja ya dharura ya hospitali ya utaalam kushughulikia visa hivyo.
“Hili ni jambo ambalo limechelewa kutekelezwa. Kituo hiki kitasaidia kutatua visa vinavyoongezeka vya matatizo ya akili,” alisema Rais Kenyatta.
Ujenzi wa hospitali hiyo yenye vitanda 600, utaanza katikati ya mwezi Juni katika kipande cha ardhi ya hekari 80 katika Eno la Karen/Ngong.
Licha ya kutoa matibabu ya Afya ya akili, hospitali hiyo iliyo na uwezo wa kuwahudimia wagonjwa 1000 wa kuingia na kutoka, pia itahifadhi chuo cha mafunzo kwa wahudumu wa afya ya akili.
Rais Kenyatta aliishukuru GKSD kwa kukubali kushirikiana na Kenya kujenga hospitali hiyo, akisema kuwa msasda wao utapanua uwezo wa Kenya wa kushughulikia visa vinavyoongezeka vya matatizo ya akili.
Kwa upande wake Ghribi alimhakikishia Rais Kenyatta kwamba shirika lake limejitolea kuisaidia Ke ya kuafikia lengo lake la kutoa huduma bora na nafuu za afya ya akili sio tu kwa raia wa Kenya pekee, mbali pia kwa raia wa kigeni kutoka kanda hii.
“Tumejitolea kuhakikisha huduma bora za afya. Kama shirika tutahakikisha kituo hiki kinaafikia viwango vya kimataifa katika utoaji matibabu ya Afya ya akili barani Afrika na kote duniani,” alihakikisha Ghribi.
Mkutano huo pia ulihudhiriwa pia na waziri wa afya Mutahi Kagwe na mkuu wa utumishi wa umma Joseph Kinyua.