Serikali imezindua utumiaji wa mtambo wa kiteknolojia wa kukabiliana na janga la corona ili kutumika kufuatilia viwango vya joto vya mwili na kukusanya takwimu za hadi watu 200 kwa dakika moja.
Mpango huo ambao ni kwanza wa shirika la umoja wa mataifa kuhusu Maendeleo ni mkakati wa kuepusha hatari ili kusaidia juhudi za kitaifa za kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 hasa wakati huu ambapo kuna tishio la kutokea kwa aina mpya ya ugonjwa wa COVID-19 na hali ya kulemewa kwa mfumo wa afya.
Waziri wa afya Mutahi Kagwe amesema mitambo hiyo mitatu iliyotolewa na shirika la umoja wa mataifa kuhusu maendeleo kwa gharama ya shilingi milioni 36 itapunguza utangamano kati ya madaktari na wagonjwa.
Mitambo hiyo itawekwa katika hospitali ya Mbagathi, hospitali ya kitaifa ya Kenyatta, na katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta.
Imebainika kuwa mataifa machache hasa katika bara Asia yametumia teknolojia sawia kutokomeza ugonjwa wa Covid-19.
Utafiti uliofanywa wakati wa utoaji mafunzo kwa wahudumu wa maabara, wauguzi , na madaktari ambao watatumia teknolojia hiyo uliashiria kuwa teknolojiia hiyo ina uwezo mkubwa wa kukabiliana na ugonjwa huo.