Kamishna wa kaunti ya Isiolo, Geoffrey Omoding, ameamuru wote ambao wanatekeleza kazi ya kuchimba dhahabu katika eneo la Kom kaunti ya Isiolo wakome mara moja. Akizungumza kwenye kikao cha hadhara katika soko la Kom jana Ijumaa, Omoding alisema kwamba wachimbaji hao wanatumia mashine zenye uwezo mkubwa kutekeleza kazi zao bila kujali athari kwa mazingira.
Alisema kwamba agizo hilo litaendelea kuwepo hadi mamlaka ya kutunza mazingira yaani National Environmental Management Authority – NEMA ifanye uchunguzi kabla ya kutoa maelekezo ya jinsi ya kutekeleza kazi hiyo ya kuchimba dhahabu. Kulingana na Omoding, tayari NEMA imeelekezwa kufanya hivyo na kutoa ripoti haraka iwezekanavyo. Wote ambao wanatekeleza kazi ya kuchimba dhahabu katika eneo hilo nao, wameelekezwa watafute leseni kutoka kwa taasisi husika za serikali kabla ya kuanza kufanya kazi hiyo.
Kamishna Omoding aliongeza kusema kwamba serikali itatuma naibu kamishna wa kusimamia eneo la Kom ili kupunguza mwendo mrefu ambao wakazi hulazimika kusafiri hadi Merti umbali wa kilomita 75 kutafuta huduma za serikali. Kuhusu maafisa wa GSU waliotumwa katika eneo hilo hivi maajuzi, Omoding alisema kwamba wamezoea eneo hilo huku akifichua kwamba waliotumwa kuhudumu katika maeneo ya Mlango na Attan watafika huko hivi karibuni.
Machifu na manaibu wao walielekezwa washirikiane na wazee wa jamii katika kuhamasisha jamii kusalimisha silaha wanazomiliki kinyume cha sheria.