Kundi linaloshirikisha mashirika mbalimbali limeharibu bidhaa za magendo za thamani ya shilingi milioni 3.3 zilizonaswa kwa kipindi cha miaka minne iliyopita, katika juhudi za kuzuia kuingizwa kwa bidhaa hizo katika kaunti ya Garissa.
Bidhaa hizo zilizoharibiwa katika jaa moja la Garissa kufuatia maagizo ya mahakama, zilijumuisha magunia 295 ya sukari ya kahawia, maziwa ya unga, viatu vya wanawake, nguo, vifaa vya urembo na dawa za kupunguza maumivu.
Akiongea wakati wa shughuli hiyo, naibu kamishna wa kaunti John Marete alisema kuwa bidhaa zilizoharibiwa zilikuwa zinahatarisha afya ya wakazi kwa vile zilikuwa hazijakaguliwa na shirika la ukadiriaji ubora wa bidhaa hapa nchini-KEBS.
“Bidhaa hizi si salama kwa matumizi ya binadamu. Ndio maana tunaziharibu ili kutuma ujumbe mkali kwa wale wanaojihusisha na biashara ya bidhaa za magendo kwamba siku zao zimekaribia,” alisema Marete.

Marete alitoa wito kwa wakazi kuwa makini wakati wanaponunua bidhaa na kuhakikisha kuwa zina alama au nembo za shirika la KEBS ambayo inadhibitisha uhalali wake.
Marete alitoa hakikisho kwa biashara halali katika eneo hilo kuwa serikali haitalegeza juhudi za kuhakikisha kuwa bidhaa za magendo haziingii katika masoko ya humu nchini.
Mnamo mwaka 2021 alipozuru kaunti ya Garissa, waziri wa usalama wa kitaifa Dkt. Fred Matiang’I, aliagiza asasi za usalama katika eneo la kaskazini mashariki mwa nchi, kukabiliana vilivyo na biashara ya bidhaa za magendo.