Serikali imeelezea wasi wasi kuwa makundi fulani ya watu hayako tayari kupeleka watoto wao kwa chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio.
Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema makundi hayo yako katika sehemu mbali mbali za nchi ikiwemo Kaunti ya Kitui.
Kagwe amekariri kuwa huduma za afya kama vile chanjo ni haki ya watoto. Alisema serikali itachukua hatua mwafaka ikiwemo kutekeleza sheria ya afya ya umma ili kuhakikisha watoto wote na Wakenya wanafurahia haki zao za kimsingi.
Kagwe ameondolea mbali hofu kuhusu usalama wa chanjo hiyo ya kuzuia ugonjwa wa kupooza, akisema chanjo zote za kuzuia ugonjwa huo zimefanyiwa uchunguzi na ziko salama kwa watoto.
Serikali inalenga kuchanja watoto milioni 3.4 dhidi ya ugonjwa wa kupooza kwenye kampeni ya chanjo itakayotekelezwa kuanzia Jumamosi wiki hii hadi Jumatano wiki ijayo.
Chanjo hiyo itatolewa katika kaunti za Mandera, Isiolo, Wajir, Garissa, Lamu, Tana River, Kilifi, Mombasa, Kitui, Machakos, Kajiado, Kiambu na Nairobi.