Jaji Mkuu, ambaye amestaafu rasmi, David Maraga amesisitiza umuhimu wa sheria kuheshimiwa ili kuhakikisha kwamba Wakenya wanaishi katika hali ya usalama humu nchini.
Akiongea wakati wa hafla maalum ya kuadhimisha kustaafu kwake Jumatatu, Maraga amewahimiza wenzake katika Idara ya Mahakama wasifanye makosa ambayo yanaweza kupeleka nchi hii katika vita.
“Majaji wenzangu, wananchi wa Kenya wamewapa mamlaka ya kuwa waangalizi wa katiba yetu, kuusimamia utawala wa sheria. Wanasiasa hawana mamlaka zaidi ya wale walio na mamlaka ya Idara ya Mahakama, msiwabwage Wakenya, simameni kidete na mfanye liliso sahihi. Fanyeni lililo sahihi na Mungu na wananchi wa Kenya watawatetea,” amesema Maraga.
Maraga amewahakikishia Wakenya kwamba ameacha nyuma Idara ya Mahakama iliyo thabiti, iliyo na majaji wa kujitolea huku akiwaomba wananchi kuwaunga mkono majaji hao pamoja na mahakimu.
“Lazima tuendelee kuwekeza katika idara yetu ya mahakama, tukitambua kwamba utulivu wa kisiasa katika nchi hii unaweza kuhakikishwa iwapo sheria itatawala. Bila utawala wa sheria katika nchi hii, sote tutakuwa washindwa,” akasema.
Aidha, ameishukuru Tume ya Huduma za Mahakama (JSC), Kitengo cha Usimamizi serikalini pamoja na kile cha uundaji sheria kwa yale ambayo wameyatimiza hadi kustaafu kwake.
Baada ya kuhudumu kama Jaji Mkuu kwa kipindi cha miaka mitano kamili, Maraga amestaafu akiwa na umri wa miaka 70.
Muda wake wa kuhudumu umeibua hisia mseto miongoni mwa Wakenya, huku wengine wakisema kumekuwa na changamoto chungu nzima ikiwemo vita kati ya Idara ya Mahakama na upande wa serikali wa usimamizi.
Wengine nao wanadai kwamba Maraga alihudumu vyema na atakumbukwa kwa hatua ya kihistoria ya kufutilia mbali matokeo ya kura za urais za mwaka wa 2017, kupunguza msongamano wa kesi mahakamani miongoni mwa ufanisi mwengine mbali mbali.
Maraga ndiye Jaji Mkuu wa 14 humu nchini na wa pili chini ya katiba mpya ya mwaka wa 2010, baada ya kuchaguliwa mnamo mwaka wa 2016 kufuatia kustaafu mapema kwa aliyeshikilia nafasi hiyo Willy Mutunga.
Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu anatarajiwa kuchukua hatamu kama Kaimu Jaji Mkuu kwa muda usiozidi miezi sita hadi nafasi hiyo itakapojazwa kwa mujibu wa sheria.