Shilole na Rommy wafunga ndoa

Mwanamuziki wa Tanzania Shilole kwa jina halisi Zena Yusuf Mohammed na mpenzi wake Rajab Issa maarufu kama Rommy3d ambaye ni mpiga picha wamefunga ndoa.

Shilole alichapisha picha moja tu ya tukio hilo akisema kwamba wamemaliza salama na kwamba sasa anaweza kuitwa “Mrs Rajab Issa”.

Arusi hiyo haikutangazwa sana ilivyokawaida ya watu maarufu nchini Tanzania na imejiri wakati ambapo waisilamu wakiwemo Shishi na Rommy wanaadhimisha mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Mwezi Januari wakihojiwa na Zamaradi Mketema, wapenzi hao walifichua kwamba wangefunga ndoa kabla ya mwaka huu kufika mwisho lakini arusi imefanyika mapema kuliko matarajio ya wengi.

Rommy3d alimvisha Shilole pete ya uchumba mwisho wa mwaka jana kwenye sherehe ya siku yake ya kuzaliwa baada ya kumvua ya zamani ambapo Shilole alibubujikwa na machozi akisema ameteseka sana.

Baadaye kuliibuka tetesi kwamba Shilole alijinunulia pete hiyo kwani Rommy3d hawezi kumudu bei yake.

Mpiga picha huyo rasmi wa Shilole alisema kwamba alijuana na Shilole kama miaka 11 iliyopita wakati alikuwa muigizaji naye akawa anatumika kama mtu wa kushika taa katika maandalizi ya filamu ambayo Shilole alikuwa anaigiza.

Mwaka 2009 Shilole na Rommy3d walikuwa na uhusiano wa kimapenzi ambao ulidumu kwa muda wa mwaka mmoja. Uhusiano huo ulifika mwisho kutokana na kile wanachokitaja kuwa changamoto za maisha.

Wawili hao wameanza uhusiano wa kimapenzi baada ya Shilole kuachana na Uchebe ambaye alikuwa akimdhulumu ilhali yeye ndiye alikuwa anamtunza.

Rommy3d ni mpiga picha wa kampuni changa ya muziki ya Shilole ambayo alizindua mwaka jana na ina msanii mmoja kwa jina Pablo Chill.

  

Latest posts

Filamu ya Kenya yashinda tuzo nchini Nigeria

Tom Mathinji

Just A Band yarejea tena baada ya kimya cha muda

Tom Mathinji

Yul Edochie Azungumzia Ndoa Yake ya Wake Wawili

Marion Bosire

Tovuti hii inatumia kuki kukuhudumia vyema. Tafadhali kubali kupokea. Kubali Fahamu Zaidi