Muigizaji na mtayarishaji wa filamu wa Marekani Spike Lee kupitia kwa kampuni yake ya 40 Acres and a Mule Filmworks, anashirikiana na kampuni ya kuunda na kuuza filamu HBO kuunda filamu ya matukio halisi ya mashambulizi ya tarehe 11 mwezi Septemba mwaka 2001 dhidi ya Marekani maarufu kama “The 9/11 NYC Attack”.
Mashambulizi hayo yalitelekezwa na makundi ya waasi na yalisababisha vifo 2,977 na watu wapatao elfu 25 wakasalia na majeraha huku mali ya pesa nyingi ikiharibiwa.
Filamu hiyo ni ya kuadhimisha miaka 20 tangu mashambulizi hayo kutekelezwa na imepatiwa mada ya “NYC EPICENTERS 9/11→2021½”.
Wahusika wameitaja kazi hiyo kuwa maelezo bayana ya uhai, hasara na kubahatika kuishi baada ya mashambulizi hayo hasa katika jiji la New York kwa muda wa miaka 20 sasa.
Itakuwa onyesho la jinsi watu wa New York wanatapatapa na kujikaza kujijenga tena baada ya shambulizi la kigaidi na wanavyojisukuma wakati huu wa janga la ulimwengu mzima la Corona.
Filamu hiyo ni historia ambayo itakuwa na picha za hali ilivyokuwa na ushuhuda wa wananchi wa tabaka mbali mbali na itapatikana kwenye jukwaa la HBO Max mwaka huu.
Spike Lee, kwa jina lingine Shelton Jackson ni mkazi wa Nwy York na anahisi kwamba ana uhusiano wa kipekee na kazi hii ya sanaa na anajivunia kushirikiana na kampuni ya HBO.
Lee alifichua kwamba watu wapatao 200 wamehojiwa kwa ajili ya kujenga filamu hiyo ya matukio halisi na wanatafuta kujua ni kwa nini Jiji la New York ni la kipekee na wakazi wake ambao wanalifanya kuwa hivyo.
Lisa Heller na Nancy Abraham, ambao wanasimamia kitengo cha filamu za matukio halisi chini ya kampuni ya HBO walisema kwamba wanafurahia kuwa na kazi nyingine ya kipekee na Spike Lee.
Wawili hao walisema wanathamini uwezo wa Spike Lee wa kuorodhesha na kusimulia matukio kutokana na kazi yake ya kusimulia kuhusu kimbunga cha Katrina huko New Orleans na sasa mashambulizi ya 9/11 mjini New York.