Tendabelua la mgombea mwenza wa Urais katika muungano wa Kenya Kwanza

Huku Muungano wa Muumgano wa Azimio la Umoja – One Kenya  ukibuni jopo la kumteua mgombea mwenza mfaafu wa Raila Odinga, kwa upande mwingine, Muungano wa Kenya Kwanza haujatangaza hadharani kuhusu mchakato wake wa kumteua mgombea mwenza.

Hali hiyo imesababisha wengi kuwa na dhana tofauti kuhusu ni nani atakuwa mgombea mwenza, kati ya wanasiasa tajika katika muungano huo.

Licha ya kuwa Kenya kwanza wanafahamu kuwa tarehe 16 mwezi Mei ndiyo tarehe ya mwisho kumtangaza mgombea mwenza, muungano huo umesalia kimya kama maji mtungini kuhusu ni nani bora zaidi kwa wadhifa huo.

Muungano huo ambao una zaidi ya vyama tanzu kumi ndani yake, unaghubikwa na kibarua kigumu cha kumteua mgombea mwenza wa Ruto bila kusambaratisha muungano huo.

Baadhi ya viongozi wanaomezea mate wadhifa wa mgombea mwenza katika Muungano wa Kenya kwanza ni pamoja na Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki, Spika wa bunge la kitaifa Justin Muturi, Gavana wa Kirinyaga Ann Waiguru na mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua miongoni mwa wengine.

Atakayechaguliwa katika wadhifa huo, kulingana na wachanganuzi wa kisiasa hapa nchini, huenda akazidisha umaarufu wa muungano huo, au kuudidimiza zaidi.

Also Read
Zaidi ya watoto 250,000 kupokea msaada wa chakula huko Kilifi

Wawaniaji wadhifa wa Urais katika uchaguzi mkuu ujao, wameonekana kuwa makini sana kuhakikisha chaguo la mgombea mwenza halisababishi nyufa chamani ama katika muungano husika, huku wanasiasa tajika wakimezea mate wadhifa huo.

Usawa wa jinsia katika wadhifa huo wa mgombea mwenza pia ni swala muhimu ambalo linaangaziwa, hasaa na makundi ya kutetea usawa wa kijinsia.

Muwaniaji Urais wa Kenya Kwanza naibu Rais William Ruto katika mkutano wa kisiasa kaunti ya Busia.

Katika Kenya Kwanza Gavana wa Kirinyaga Ann Waiguru, ndiye mwanamke wa kipekee anayemezea mate wadhifa huo na kumweka katika nafasi bora ya kuteuliwa iwapo muungano huo utaazimia kumtea mgombea mwenza wa kike.

Makundi kadhaa yamejitokeza kumuunga mkono Waiguru kuwa mgombea mwenza wa Ruto.
kundi moja la vijana wa muungano huo lilijitokeza na kusema kimasomaso kuwa linampendekeza Ann Waiguru kuwa mgombea mwenza wa Dkt. William Ruto.

Vijana hao kutoka kaunti zote 47 hapa nchini, kutoka vyama tanzu sita ndani ya muungano wa Kenya Kwanza, walikuwa wakizungumza katika kaunti ya Nakuru.

Also Read
Ruto asifu mjadala wa kisiasa unaoangazia kuboresha uchumi

Kulingana na kundi hilo la vijana, Gavana huyo wa Kirinyaga, ana tajiriba ya kupigiwa mfano, kutokana na utendakazi wake kwa Wakenya.

“Waiguru ameshikilia nyadhifa muhimu sana ikiwemo katika hazina kuu, na pia akiwa waziri ameonyesha ana uwezo wa kuongoza serikali,” alisema mwenyekiti wa vijana wa Kenya Kwanza tawi la Kakamega Barbara Juma.

Vijana hao walidai kuwa chaguo la Waiguru, litawavutia wapiga kura wengi wa kike, na kusaidia Kenya Kwanza kutwaa ushindi wa kiti cha Urasi katika uchaguzi mkuu ujao.

“Muungano utakaokuwa na mgombea mwenza mwanamke, utavutia wapiga kura wa kike na utaungwa mkono na wakenya wengi,” alisema Barbara

Kwa upande mwingine, Kithure Kindiki ametajwa kuwa bora zaidi kuwa mgombea mwenza wa William Ruto katika kinyang’anyiro hicho cha Urasi mwezi Agosti mwaka 2022.

Profesa huyo ambaye alikuwa miongoni mwa mawakili wa naibu Rais katika mahakama ya maswala ya uhalifu mjini the Hague, aliweka kando azma yake ya kuwania ugavana wa Tharaka Nithi ili kujishughulisha na kampeni za kitaifa za muungano wa Kenya Kwanza.

Also Read
Polisi wakomesha mkutano wa kisiasa Kitui

Hatua hiyo ya Kindiki ya kutupilia mbali azma ya ugavana wa Tharaka Nithi, kuliwapa wengi dhana kwamba huenda akachaguliwa kuwa mgombea mwenza wa Dkt William Ruto.

Kindiki hajazungumza hadharani kuhusu ufaafu wake kushikilia wadhifa huo wa kumezewa mate, lakini wanadani wake wanaashiria huenda akakabidhiwa jukumu hilo.

Kutokana na kutokuwepo hadharani kwa mchakato utakaofuatwa na Kenya Kwanza kumtafuta mgombea mwenza bora, haijabainika iwapo mgombea mwenza huyo atakuwa wa kike au kiume, licha ya kuwa makundi mengi ya kutetea usawa wa kijinsia yakipendekeza kuwa mgombea mwenza wa Urais anapaswa kuwa mwanamke.

Wakenya wanasubiri kwa hamu na ghamu kuona iwapo wagombea urais katika uchaguzi mkuu ujao watawateua wagombea wenza wa jinsia tofauti. Iwapo hilo litatekelezwa, basi itakuwa ni historia kwa taifa hili kwa kuwa na naibu Rais wa kwanza mwanamke.

Macho yote sasa yameelekezwa kwa wawaniaji Urais kuona iwapo wataweka historia mpya kwa taifa hili, ikizingatiwa zimesalia siku chache tu kabla ya kukamilika kwa makataa ya kuwasilisha majina ya wagombea wenza wa Urais na Ugavana.

  

Latest posts

Dereva na Makondakta wawili watiwa nguvuni kwa kukiuka sheria za trafiki

Tom Mathinji

Watu wanne zaidi wameambukizwa Covid-19 hapa nchini

Tom Mathinji

Matabibu wataka Uchunguzi wa mipakani kuimarishwa kuzuia kuenea kwa Ebola

Tom Mathinji

Tovuti hii inatumia kuki kukuhudumia vyema. Tafadhali kubali kupokea. Kubali Fahamu Zaidi