Jacques Bermon Webster II maarufu kama Travis Scott ni mwanamuziki wa mtindo wa rap nchini Marekani na amegonga vichwa vya habari baada ya kutoa usaidizi wa masomo kwa wanafunzi wapatao 100 wanaosomea kwenye taasisi na vyuo ambavyo vinaaminika kuwa vya watu weusi nchini humo yaani HBCUs. Travis alitoa usaidizi huo kupitia wakfu wake wa Cactus Jack Foundation na alitangaza jana Jumanne kwamba walionufaika wanastahili kufuzu mwaka huu wa 2022.
Usaidizi huo wa kimasomo ni sehemu ya mpango wa “Project HEAL” wake Travis alioutangaza mwezi machi na sehemu ya pesa zilizopatikana ziliwekwa kando kwa matumizi ya usaidizi wa kimasomo. Kupitia usaidizi huo wa Scott hazina ya usaidizi wa kimasomo ya Waymon Webster imetoa usaidizi wa dola elfu kumi kwa wanafunzi wa HBCU. Usaidizi unalenga wanafunzi werevu na ambao hawana uwezo wa kifedha ili waweze kukamilisha masomo na kufuzu kwa wakati. Waymon Webster ni jina la babu yake Travis ambaye alikuwa mwanafunzi wa mojawapo ya taasisi za watu weusi na mhadhiri katika chuo cha Prairie View A&M University.
Kwenye taarifa yake ya kutangaza usaidizi huo, Travis alisema watu weusi ni werevu na ni bora ila hawapati fursa za kujiendeleza na ndio sababu yeye na familia yake walianzisha mpango huo wa usaidizi.
Walionufaika na usaidizi wa hivi punde wa Cactus Jack Foundation wa kimasomo ni wa vyuo na taasisi kama vile Alabama A&M University, Central State University, Florida A&M University, Jackson State University, Morehouse College, Texas Southern University, Grambling State University, Xavier University of Louisiana na Prairie View A&M University.