Tume ya mishahara na marupurpu (SRC) imekosoa mgomo wa wafanyakazi wa hospitali ya kitaifa ya Kenyatta unaolenga kushinikiza nyongeza ya mishahara ikisema mgomo huo haufai.
Kwenye taarifa kwa vituo vya habari , tume hiyo imetaja mgomo huo kuwa haramu ikisema matakwa ya wafanyakazi hao hayaambatani na ushauri wa tume hiyo kuhusu nyiongeza ya mishahara.
Tume hiyo imesema wahudumu wa afya katika hospitali hiyo tayari wameongezewa mishahara kwenye mpango wa nyongeza ya mishahara ya mwaka wa kifedha wa 2017/2018 hadi 2020/2021.
Aidha tume hiyo imesema kabla ya kuidhinisha ongezeko lolote la mishahara ipo haja ya kuhakikisha gharama ya mishahara imeshughulikia ipasavyo , kuhakikisha huduma za umma zinaweza kuvutia na kudumisha wafanyakazi wenye ujuzi unaohitajika , kutambua utendsakazi bora , kuhakikisha uwazi na haki na malipo sawa kwa wafanyakazi wote.
Tume ya SRC vile vile imesema haiwezi kuidhinisha chochote nje ya ushauri wake.
Huduma katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta zimesalia kulemazwa kwa siku ya tatu kufuatia mgomo unaoendelea wa wahudumu wa afya.
Wahudumu hao wamedumisha msimamo wao huku wakiazimia kutorejea kazini hadi tume ya SRC iidhinishe hospitali hiyo kutekeleza nyongeza hiyo ya mishahara.
Wafanyakazi wa hospitali hiyo walianzisha mgomo Jumatatu asubuhi huku wakituhumu tume ya SRC kwa kukosa kusawazisha mishahara yao.