Tuzo ya mwanaspoti bora wa mwaka (Sports personality of the year award (SOYA) ya timu bora ya mwaka kwa wanawake, itakuwa na ushindani mkali wakati wa makala ya 18 ya Soya yatakayoandaliwa uwanja wa Bukhungu kaunti ya Kakamega tarehe 25 mwezi huu.
Mabingwa wa kombe la CECAFA ,Vihiga Queens wamo kwenye kinyang’anyiro, baada ya kusajili matokeo bora mwaka uliopita ikiwemo kushiriki makala ya kwanza ya komba la ligi ya mabingwa Afrika .

Timu ya taifa ya Voliboli kwa wanawake ,Malkia Strikers pia wamo katika orodha ya kuwania tuzo hiyo ,baada ya kuwa timu pekee ya Afrika iliyofuzu kwa michezo ya Olimpiki ya mwaka jana na kisha wakanyakua nafasi ya pili kwenye mashindano ya kombe la Afrika nchini Rwanda.

Vipusa wa Voliboli ya ufukweni (Beach Volleyball) wamo katika orodha ya kuwania tuzo ya timu bora baada ya kunyakua ubingwa wa Afrika na kufuzu kwa michezo ya Olimpiki kwa mara ya kwanza mjini Tokyo Japan.
Wengine wanaowinda tuzo hiyo ni timu taifa ya raga kwa wachezaji 7 kila upande ,Kenya Lionesses walionyakua kombe la Safari Sevens,na timu mpira wa kikapu ,Kenya Lionesses iliyoshinda ubingwa wa Africa zone 5 na kufuzu kwa mashindano ya FIBA Afrobasket.

Tuzo za SOYA ambazo zinaadhimisha miaka 18 tangu kuzinduliwa zitashuhudia wanaspoti wakiwania tuzo katika vitengo vya mchezaji bora ,timu bora,mchezaji bora kwa wanawake na wanaume na mchezaji bora kwa jumla .

Makala ya mwaka huu yataandaliwa katika uwanja wa Bukhungu kaunti Kakamega,na yamefadhiliwa na kaunti ya Kakamega,Lotto Foundation,Safaricom,hazina ya malipo ya uzeeni NSSF na kampuni ya CPF Financial Services.