Mashirika ya ujasusi ya Uingereza yamenasa takriban dola milioni 5.8 zilizokuwa zimeibwa na Gavana wa jimbo moja nchini Nigeria.
Serikali ya Uingereza imeirudishia Nigeria pesa hizo ambazo ziliibwa na gavana huyo na kufichwa nchini humo.
Nigeria ilisema kuwa aliyekuwa Gavana wa Jimbo la Delta James Ibori alishtakiwa kwa ulanguzi wa pesa alizozihamishia Uingereza mnamo mwaka wa 2012.
Viongozi wa mashtaka walisema kuwa Ibori aliiba dola milioni 165 kutoka jimbo la Delta lenye utajiri mkubwa wa mafuta.
Mkuu wa sheria nchini Nigeria Abubakar Malami ameishukuru Uingereza kwa hatua hiyo, akisema imepandisha hadhi ya nchi hiyo kutokana na harakati za kurudisha mali iliyoibwa.
Wachanganuzi wa maswala ya kiuchumi wamesema serikali imepania kutwaa pesa zaidi kutoka kwa gavana huyo.
Ndege ya kibinafsi ya Gavana Ibori ni miongoni mwa mali ambazo serikali itampokonya gavana huyo.