Zaidi ya makundi mia moja ya wanawake na vijana katika wodi ya Kathama/Mbiuni katika eneo la Mwala yamepokea shilingi nusu milioni kila mmoja kutoka kwa hazina ya serikali ya taifa ya NGAAF.
Mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Machakos Joyce Kamene, amesema kuwa pesa hizo zitasaidia kuboresha shughuli mbalimbali katika makundi hayo na kuimarisha hali ya kiuchumi ya wanachama.
Akiongea katika eneo la Mbiuni, Kamene alitoa wito kwa makundi yaliyonufaika na pesa hizo kuanzisha miradi ya kuleta mapato ili kuimarisha hali ya kijamii na kiuchumi ya wanachama wake. Alitoa wito kwa wanachama kulipa mikopo yao kwa wakati.
“Fedha hizo zitawawezesha wanachama kuimarisha hali yao ya kiuchumi hasaa wakati huu ambapo uchumi wa taifa hili umevurugwa na janga la Covid-19,” alisema Kamene.
Kamene hata hivyo alilalamikia kujitokeza kwa watu wachache kujisajili kuwa wapiga kura katika kaunti hiyo huku akitoa wito kwa wale waliohitimu kujitokeza na kujisajili kwa wingi ili kuipa jamii hiyo nguvu katika siasa za kitaifa na katika uchaguzi mkuu ujao.