Vijana wanufaika pakubwa na mpango wa serikali wa uanagenzi

Kila mwaka, maelfu ya vijana huhitimu na kufuzu kutoka vyuo pamoja na vyuo vikuu mbali mbali kote nchini.

Baada ya kuandaliwa sherehe za mbwembwe za kufuzu, vijana hawa barubaru hujituma katika soko la ajira wakiwa na matumaini maridhawa ya kupata ajira katika utumishi wa umma au katika idara za serikali.

Punde tu wanapoanza pilkapilka za kutafuta ajira, hitaji ambalo waajiri wengi huitisha ni tajiriba ya kufanya kazi.

Hitaji hili kwa hakika limekuwa changamoto kuu kwa vijana wengi na nyakati nyingi hitaji hilo, husababisha vijana hawa kupoteza fursa nzuri za kuajiriwa.

Ni kutokana na changamoto hilo, ndiposa serikali  ilipotangaza mpango uliolenga kuwapa vijana wa humu nchini tajiriba ya kikazi, na kuwaweka vijana hao katika nafasi nzuri ya kuajiriwa hapa nchini.

Mpango wa uanagenzi katika utumishi wa umma, ulianzishwa mwezi Agosti mwaka 2019, na hadi kufikia sasa umewasaidia maelfu ya vijana kupata tajiriba ya kazi, ujuzi ufaao na pia kuboresha ushindani wao wanapotafuta ajira.

Wakati wa kipindi hicho cha mwaka mmoja, wanagenzi hao hupokea mafunzo kemkem kuhusu taaluma yao.

Mpango huo tangu kuanzishwa kwake, umewanufaisha Zaidi ya vijana 10,000 ambao wamepokea mafunzo kwa ufanisi wa kupigiwa mfano.

Tume ya kuwaajiri watumishi wa umma hapa nchini PSC, katika robo yake ya kwanza ya mwaka wa kifedha, kupitia magazeti ya humu nchini na pia katika mitandao yake, huchapisha tangazo la wanaotaka kujiunga na mpango huo wa uanagenzi.

Wanagenzi ambao hufaulu kujiunga na mpango huo, huelimishwa kuhusu mpango huo kabla ya kupelekwa katika idara mbali mbali za serikali ambazo zina nafasi za wanagenzi. Wanapowasili katika idara husika, wao huwasilisha stakabadhi zao kwa tume ya PSC ili wajumuishwe katika mfumo wa malipo ya mshahara.

Fauka ya hayo, wanagenzi hufanya kazi sako kwa bako na washauri wa maswala ya utaalam na ujuzi wa maisha. Mpango huo wa uanagenzi unalenga kuwakuza vijana hao kuwa wananchi wazalenzo, waaminifu na waadilifu.

Mpango huu wa uanagenzi unatekeleza jukumu muhimu katika kupiga jeki ajenda nne kuu za Rais Uhuru Kenyatta kupitia ajira kwa vijana.

Also Read
Uhuru Kenyatta: UNCTAD inauwezo wa kukwamua uchumi wa ulimwengu

Na ili kuhakikisha ubora na viwango vya juu vya mpango huo vinadumishwa, tume ya kuwaajiri watumishi wa umma PSC, imetoa mafunzo kwa maafisa wake kutoka idara mbali mbali kuwa wakufunzi wa wanagenzi hao.

Wanagenzi hawa hupata fursa nzuri ya kuwa na taswira halisi ya taaluma yao katika utumishi wa umma, kuboresha utaalam wao na kupata nafasi za kukuzwa kitaalam.

Katika wakilishi wadi ya Kapchok, eneo bunge la Kacheliba, tunakutana na Jesse Rotich akiwa katika mojawepo ya mikutao yake ya uhamasisho.

Rotich ambaye anafanya kazi katika wizara ya afya ya kaunti hiyo akiwa afisa wa afya, amekuwa akishirikiana na jamii hii kwa muda wa miezi kadhaa.

Kulingana na Rotich, kazi hiyo ya afisa wa afya aliipata kutokana na ujuzi kupitia mpango wa serikali wa uanagenzi, uliomweka kifua mbele alipokuwa akituma maombi ya kazi katika serikali ya kaunti ya Pokot Magharibi.

Anasema tangu alipohitimu kutoka chuo kikuu cha Kenyatta mwaka 2015, amekuwa na ugumu wa kupata kazi, akidokeza kuwa ni kutokana na ukosefu wa tajriba ya kazi ambayo ilikuwa hitaji kutoka kwa waajiri wengi

Rotich anatoa wito kwa vijana wenzake kuchukua fursa ya mpango huo, huku akiwahimiza wale ambao bado hawajabahatika kuchukuliwa katika mpango huo, kutokufa moyo na kuendelea kutuma maombi ya kuwa mwanagenzi.

Kijana huyu anaelezea furaha isiyo na kifani kutokana na jukumu lake analotekeleza kusaidia jamii na taifa kwa jumla, la uhamasisho kuhusu mbinu bora za afya katika jamii na kusaidia kuimarisha huduma za afya kwa wote.

Mercy Ng’iro, ambaye ni afisa mkuu wa afya katika kaunti ndogo na ambaye pia ni msimamizi wa Rotich, alisema tajriba ya Rotich ilimfanya kuwa bora Zaidi miongoni mwa wengine wengi waliokuwa wakimezea mate kazi hiyo.

Ng’iro alisema mpango huu wa uanagenzi unatekeleza wajibu muhimu katika kuwanoa makali vijana kuwa watumishi a umma wa kupigiwa mfano.

Kutoka kaunti ya Pokot Magharibi, moja kwa moja tulifululiza na kutua Magharibi mwa taifa hili, kaunti ya Bungoma. Katika kituo cha mafunzo ya kilimo cha Mabanga, tunampata Phillis Mutoro akichapa kazi kwa bidii za mchwa. Mutoro ambaye pia amenufaika kwa mpango huu wa uanagenzi, kwa sasa ameajiriwa kuwa meneja wa shamba wa taasisi hiyo.

Also Read
Rais Kenyatta: Kenya na Somalia zitashirikiana kudumisha amani

Kulingana naye, tajriba aliyopokea wakati wa kipindi cha mwaka mmoja cha uanagenzi, ilimweka katika nafasi bora alipokuwa akitafuta ajira.

Mutoro alidokeza kuwa wasimamizi wao wakati wa kipindi cha uanagenzi, walitekeleza wajibu muhimu wa kumfanya kuwa mfanyikazi wa kupigiwa mfano.

Phyllis ambaye ni mtaalam wa sayansi ya mimea kutoka chuo kikuu cha Nairobi, anafurahia kazi yake, akisema hilo lilikuwa azimio lake tangu alipokuwa mchanga.

Kwa sasa maelfu ya vijana kote nchini wamesajiliwa katika mpango huo wa uanagenzi kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kelvin Kimani, ambaye pia amenufaika na mpango huo, kwa sasa yuko katika taasisi ya utafiti wa misitu hapa nchini kaunti ndogo ya Turbo, chini ya mpango huo wa uanagenzi. Kimani aliyehitimu na shahada ya uzamili katika maswala ya kawi kutoka chuo kikuu cha Hariot-Watt nchini Uingereza.

Kevin Kimani mwanagenzi kupitia mpango wa serikali.

Kimani anasema kuwa mpango huo utamsaidia pakubwa katika kuhamasisha utandu wa misitu hapa nchini na kumpa tajriba inayohitajika kuelezea ajenda hiyo miongoni mwa vijana wenzake.

Lengo la Kimani ni kuwa mfano bora kwa vijana wa humu nchini ambao alisema wamo katika nafasi nzuri ya kusaidia taifa hili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya anga.

Kwa mujibu ya kijana huyu mtanashati, akiwa katika taasisi hiyo ya utafiti wa misitu, ataweza kutekeleza yale aliyoyasoma akiwa katika chuo kikuu.

Licha ya kupokea mafunzo ya kiufundi, mwanasayansi huyu mchanga, anasema akiwa katika mpango huu wa uanagenzi, ameweza pia kujifunza mengi kuhusu ujuzi wa maisha.

Anapongeza mpango huu wa serikali ambao anasema umebadilisha maisha ya vijana wengi hapa nchini.

Mwanamazingira mwingine mchanga ni James Clinton Kianga mwenye umri wa miaka 27, ambaye ametumwa katika halmashauri ya usimamizi wa mazingira NEMA kaunti ya Machakos, chini ya mpango wa uanagenzi, Kianga aliyehitimu kutoka chuo kikuu cha Masaai Mara, anasema amekuwa na ari kuhusu uhifadhi wa mazingira.

Katika afisi ya NEMA iliyoko Machakos, Kianga jukumu lake ni kutoa leseni kwa wateja wanaotekeleza miradi kadhaa katika kaunti hiyo. Anaelezea furaha yake isiyokifani kuhusu wajibu wake wa uhifadhi wa mazingira.

Also Read
Mwezi mtukufu wa Ramadhan kuanza wikendi hii

Kupitia mpango huu wa uanagenzi, mtetezi huyu wa mazingira, anasema ameweza kujisaidia na pia kupiga jeki familia yake.

Wasimamizi wake wanasema kuwa mpango huu utaimarisha pakubwa utumishi wa umma, kwa kuwa wakati wa kipindi chao cha uanagenzi, vijana hawa hutekeleza majukumu sawia nay ale ya wafanyikazi walioajiriwa.

Na katikati ya mji wa Embu, William Mwangi yuko katika pilka pilka za kutekeleza majukumu yake ya kila siku. Mwangi ni mtanashati mwanagenzi katika kampuni ya umeme afisi ya Embu. Yeye ni mhandisi wa umeme kutoka chuo cha kiufundi cha Kenya.

Mhandisi huyu mchanga wa umeme anasema ana matumaini ya siku njema za halafu kwa kuwa mpango huu wa uanagenzi unamuandaa kwa soko la ajira. Anasema tajiriba anayoipokea itamweka katika nafasi nzuri ya ushindani.

James Clinton mwanagenzi katika halmashauri ya NEMA kaunti ya Machakos.

Sawia na wenzake katika mpango huu, Mwangi anamatumaini kuwa mpango huu wa uanagenzi utendelea na serikali ijayo, ili kuwasaidia vijana wengine walio katika vyuo na vyuo vikuu kila mwaka.

Mwangi alisema mpango huu ni tofauti kabisa na mipango mingine aliyoshiriki ya uanagenzi, kwa kuwa kando na tajriba anayopokea fedha anazopata wakati wa kipindi hicho cha mwaka mmoja, zimemsaidia kujikimu na kuwapunguzia mzigo wazazi wake.

Katika afisi ya naibu chansela wa chuo kikuu cha Eldoret, Praxide Kimutai yuko nyuma ya tarakilishi akifanya kazi zake za kila siku. Kimutai ambaye alihitimu kutoka chuo kikuu cha Karatina, alisomea usimamizi na mipango ya miradi. Akiwa katika mwezi wake wa kwanza katika mpango huu wa uangenzi, Kimutai anashikilia kuwa alifanya uamuzi wa busara kuchukua fursa hiyo ya uanagenzi.

Kimutai anawashukuru wanafunzi wenza katika chuo hicho kikuu, anaosema wamemsaidia sana katika taasisi hiyo na wanaoendelea kumpa matumaini katika kazi hiyo.

Ni bayana kwamba mpango wa uanagenzi ulioanzshwa na Rais Uhuru Kenyatta umebadilisha pakubwa maisha ya maelfu ya vijana wa hapa nchini na ujuzi watakopata utawawezesha kupata ajira katika soko la ajira lililo na ushindani mkubwa.

 

  

Latest posts

Ajali ya kwanza yatokea katika barabara ya Expressway

Tom Mathinji

Rais Kenyatta akamilisha kongamano la Jumuiya ya Madola Rwanda

Tom Mathinji

Waziri Matiang’i: Tutakabiliana vilivyo na makundi ya Majambazi

Tom Mathinji

Tovuti hii inatumia kuki kukuhudumia vyema. Tafadhali kubali kupokea. Kubali Fahamu Zaidi