Vurugu zilishuhudiwa jijini Jerusalem nchini Israel Ijumaa wakati watu wengi walijitokeza kuhudhuria mazishi ya mwanahabari wa muda mrefu wa Al Jazeera Shireen Abu Akleh. Akleh aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa anaripoti kuhusu uvamizi wa jeshi katika kambi moja ya wakimbizi kwenye mji wa Jenin.
Waombolezaji walitembea kutoka eneo la Jaffa Gate hadi makaburi ya Mount Zion. Maafisa wa polisi wa Israel ambao walikuwa wamejipanga nje ya hospitali ya hospitali ya St. Joseph walikabiliana na waombolezaji hao walipojaribu kubeba jeneza la mwanahabari huyo ambalo wakati mmoja lilionekana kudondoka kutoka kwa mikono yao. Mwili wa Abu Akleh ulizikwa karibu na ilikozikwa miili ya wazazi wake huku kengele za kanisa zikikirizwa kwenye makaburi hayo. Mazishi yalijiri siku moja baada ya matembezi ya watu wengi hadi mjini Ramallah kwa ajili ya kumkumbuka.
Waumini wa kiisilamu waliokuwepo walifanya sala zao za Ijumaa kama kawaida na baadaye wakasikika wakiimba nyimbo za kuhimiza wengine kwamba watembee kwa miguu wakiwa wamebeba mwili wa Shireen hadi kanisani. Ibada ya mazishi ilifanyika katika kanisa Katoliki la eneo hilo kabla ya kuelekea makaburini kwa mazishi.
Shireen Abu Akleh ni mwanahabari ambaye alizaliwa jijini Jerusalem nchini Israel na ambaye pia alikuwa na uraia wa Marekani. Amekuwa akifanya kazi kama ripota wa lugha ya kiarabu kwenye kampuni ya Aljazeera kwa muda wa miaka 25. Anachukuliwa na wengi kuwa sauti ya wapalestina.