Shughuli katika kaunti ya Homa Bay zilitatizwa baada wafanyikazi wa serikali ya kaunti hiyo kugoma, kulalamikia kucheleweshewa mishahara yao ya miezi miwili.
Huku wakiandamana nje ya afisi za Gavana wa kaunti hiyo Cyprian Awiti, watumishi hao wa umma walisema hawatarejea kazini hadi mishahara yao ya miezi ya Aprili na Mei itakapolipwa.
Katibu wa chama cha wafanyikazi wa serikali za kaunti tawi la Homa Bay Meshack Onyango, alisema serikali ya kaunti ya Homa Bay ilikiuka makubaliano yaliyowekwa hapo awali kuhusiana na malipo ya mishahara.
“Tutaendelea kukusanyika hapa katika afisi za Gavana hadi mishahara hiyo ya miezi miwili itakapolipwa. Makubaliano yoyote kuhusu ulipaji mishahara hadi sasa hayajaafikiwa,” alilalamika Onyango.
Katibu wa chama cha watumishi wa umma tawi la Homa Bay Tom Mboya Aketch, alisema hawatarejea kazini hadi walipwe mishahara yao.
“Hatutarejea kazini hadi tulipwe mishahara yetu iliyocheleweshwa. Wanapaswa kuwasiliana na maafisa chama chetu ili kutia saini mkataba wa kurejea kazini,” alifoka Aketch.
Mkataba wa kurejea kazini uliotiwa saini mwaka 2021 na chama hicho cha wafanyikazi na serikali ya kaunti ya Homa Bay, ulidokeza kuwa mishahara ya wafanyikazi italipwa tarehe nane ya kila mwezi, lakini kulingana na wafanyikazi hao, serikali ya kaunti ya Homa Bay imezembea kutekeleza hayo.