Wahudumu wa afya wa hospitali ya kitaifa ya Kenyatta wamegoma kushinikiza tume ya mishahara na marupurupu SRC kutekeleza nyongeza ya mwaka 2012 ya mishahara yao.
Mgomo huo ulioanza usiku wa kuamkia Jumanne umelemaza shughuli katika hospitali hiyo.
Wahudumu hao waliandamana nje ya vitengo vya kushughulikia masuala ya dharura na waathiriwa wa ajali na pia vitengo vya kutibu majeruhi wakibeba mabango.
Wahudumu hao wameazimia kutotoa huduma zao hadi matakwa yao yatakapo tekelezwa.
Wamesema tume ya SRC inafaa kutekeleza nyongeza hiyo ya mwaka 2012 ili wasitishe mgomo huo.
Mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha kitaifa cha wauguzi hapa nchini Alfred Obenga ametuhumu tume ya SRC kwa kukosa kusawazisha mishahara hiyo licha ya mashirika kadhaa ya serikali kutoa idhini ya kufanya hivyo.
Obenga amesema mishahara ya wafanyakazi hao haijaongezwa tangu mwaka 2012.
Wakati huo huo , mkutano ulioitishwa na wizara ya leba ili kutatua mzozo huo wa mishahara unaendelea.