Baadhi ya vijana waliokamatwa na maafisa wa polisi kwa tuhuma za kuwa wanachama wa genge la Panya Road ambalo limekuwa likihangaisha wakazi wa jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania walifikishwa mahakamani jana Ijumaa. Mtuhumiwa wa kwanza kwa jina Daud Abdallah wa umri wa miaka 22, mkazi wa Tungini na wenzake 16 walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Fadhili Luvinga kusomewa mashtaka manane yanayowakabili.
Waendesha Mashtaka walidai kuwa Watuhumiwa kwa pamoja walitenda makosa hayo tarehe 24 mwezi Aprili mwaka huu katika eneo la Chanika Ilala jijini Dar es Salaam na bado wengine wanatafutwa. Washukiwa wote walikana mashtaka dhidi yao na kesi ikaahirishwa hadi tarehe 27 mwezi huu na wakarudishwa rumande.
Vijana hao walikamatwa na maafisa wa Polisi jijini Dar es Salaam yapata siku saba zilizopita baada yao kutekeleza uhalifu kama vile wizi wa kimabavu dhidi ya watu wengi katika sehemu tofauti za jiji hilo. Taarifa kutoka kwa msimamizi wa polisi jijini Dar es Salaam Jumanne Muliro, iliarifu kwamba oparesheni ya kukamata wanachama wa genge hilo imekuwa ikiendelea tangu Aprili 27.
Wanachama wa kundi hilo wanasemekana kuwa wa umri wa kati ya miaka 13 na 20 na walipokamatwa walipatikana na silaha kama mapanga, visu na makasi makubwa vitu ambavyo wanatumia kutekeleza uhalifu. Taarifa ya polisi inafafanua kwamba maafisa wa polisi walihoji wakaazi wa maeneo kadhaa ya Dar es Salaam na wakafanikiwa kutambua washukiwa wa visa vya uhalifu. Maafisa hao walipata pia vitu vinavyodhaniwa kuibwa kutoka kwa washukiwa zikiwemo runinga 12 na simu za rukono nne.