Huku idadi ya maambukizi ya virusi vya Covid-19 ikiendelea kuongezeka hapa nchini, sasa wizara ya afya imesema kuwa wanawake wajawazito wanaweza kupata chanjo za Pfizer au Moderna katika kipindi chochote cha uja uzito wao.
Hatua hiyo ya serikali ni katika juhudi za kudhibiti msambao wa virusi hivyo hatari hapa nchini.
Wizara hiyo imesema kuwa kupata chanjo hizo ni muhimu katika kuepusha maambukizi ya COVID-19 kwa wanawake wajawazito.
Hata hivyo wizara hiyo imesema kuwa wanawake wajawazito walioanza kupata aina nyingine za chanjo wanafaa kukamilisha chanjo hizo.
Serikali imesema kuwa chanjo ya Pfizer pia imeidhinishwa kwa vijana walio na umri wa zaidi ya miaka 15.
Serikali inalenga kuwachanja watu milioni kumi dhidi ya Covid-19 kufikia mwishoni mwa mwaka 2021.
Kwa sasa dunia nzima inashuhudia msambao wa aina ya Omicron ya Covid-19, huku safari za ndege kutoka kusini mwa Afrika kuelekea mataifa ya ulaya zikisitishwa.
Uingereza na Marekani pia zinajizatiti kukabiliana na idadi ya juu ya maambukizi ya Omicron, huku Marekani ikisema itawapima Covid-19 watu milioni 500 bila malipo ili kusaidia kuzuia msambao wa ugonjwa huo.