Makala ya 18 ya tuzo za kila mwaka za Soya yamepigwa jeki , baada ya kupokea udhamini wa shilingi milioni 4 mapema Alhamisi, huku hafla ya mwaka huu ikipangwa kuandaliwa tarehe 25 mwezi huu katika uwanja wa Bukhungu kaunti ya Kakamega.
Hazina ya malipo ya uzeeni NSSF imefadhili tuzo za mwaka huu kwa kima cha shilingi milioni 2 ,wakati kampuni ya Lotto ikitoa shilingi milioni 1 unusu nayo Safaricom ikaongezea nusu milioni.

Mwenyekiti wa jopo la uteuzi wa washindi ,Chris Mbaisi amefichua kuwa matayarisho yamekamilika kwa hafla ya mwaka huu,ambapo kinyume na mwaka jana kutakuwa na zawadi ya pesa kwa washindi.
“Kama jopo tunapanga kutoa orodha ya wanamichezo watatu bora wa mwisho katika kila kitengo wiki ijayo na kila kitu kiko sawa kulingana na mpangilio,kinyume na mwaka jana ,mwaka huu kutakuwa na zawadi ya pesa kwa washindi wa kila kitengo”akasema Mbaisi

Vitengo vitakavyoshindaniwa katika tuzo za mwaka huu ni pamoja na timu bora ya mwaka kwa wanaume na wanawake,mchezaji chipukizi bora wa mwaka kwa wanaume na wanawake,mchezaji bora wa mwaka kwa walemavu kwa wanaume na wanawake,mchezaji bora wa mwaka kwa wanaume na wanawake na pia mchezaji bora wa mwaka kwa jumla.

Tuzo za Soya zilianzishwa miaka 18 iliyopita na aliyekuwa bingwa mara tano wa dunia katika mbio nyika ambaye pia ni Rais wa kamati ya Olimpiki NOCK Paul Tergat , kwa lengo la kuwatambua na kuwatuza wanamichezo wanaotia fora kila mwaka.