Kenya imenakili visa 23 vipya vya Covid-19 baada ya kupimwa kwa sampuli 2,646 katika muda wa saa 24 zilizopita. Kiwango cha maambukizi ya Covid-19 hapa nchini sasa ni cha asilimia 0.9
Idadi jumla ya visa vilivyothibitishwa hapa nchini sasa ni 323,975 kutoka kwa Idadi ya sampuli 3,628,019 zilizochunguzwa tangu mwezi Machi mwaka 2020.
Kati ya visa hivyo vipya, watu 17 ni raia wa Kenya na sita ni raia wa kigeni, huku 11 wakiwa wa kiume na12 wa kike.
Mwathiriwa mchanga zaidi ana umri wa miaka 15 na mkongwe zaidi ana umri wa miaka 58.
Wagonjwa wanne wamepona ugonjwa huo hapa nchini wote kutoka mpango wa kuwatunza wagonjwa nyumbani. Idadi hiyo inafikisha Idadi jumla ya waliopona Covid-19 hapa nchini kuwa 318,120.
Hakuna mgonjwa ambaye amefariki kutokana na Covid-19 hapa nchini katika muda wa saa 24 zilizopita, huku Idadi ya maafa ikisalia kuwa 5,649.
Kulingana na waziri wa afya Mutahi Kagwe, jumla ya wagonjwa sita wamelazwa katika hospitali mbali mbali kote nchini, huku wengine 200 wakiuguzwa wakiwa nyumbani.
Hakuna mgonjwa aliyelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi ICU, lakini wagonjwa wawili wanapokea hewa ya ziada ya Oxygen wakiwa katika wodi za kawaida.
Jumla ya watu 17,992,422 wamechanjwa dhidi ya Covid-19 kote nchini. Kati ya Idadi hiyo, watu 16,346,555 Wana umri wa miaka 18 na zaidi.
Vijana 1,296,562 walio na umri wa kati ya miaka 15 hadi 17, wamechanjwa dhidi ya Covid-19 hapa nchini.