Watu wawili wamethibitishwa kuwa wamefariki, baada ya jengo moja kuporomoka katika mtaa wa Kihunguro eneo la Ruiru kaunti ya Kiambu.
Jengo hilo lilikuwa limependekezwa kubomolewa na halmashauri ya barabara kuu nchini KENHA, ili kutoa fursa kwa upanuzi wa barabara.
Jengo hilo liliporomoka Jumatano asubuhi, na kusababisha wapangaji waliokuwa wakiishi katika sehemu ya jengo hilo kukwama.
Halmashauri ya KENHA ilikuwa imebomoa sehemu ya jengo hilo, ili kutoa fursa kwa upanuzi wa barabara ya Eastern Bypass ili kuwa ya safu mbili kwa kitita cha shilingi bilioni 12.5.
Makundi ya huduma za dharura yanaendelea na shughuli za kuwaokoa waliokwama ndani ya vufusi, huku polisi wakizingira eneo hilo.