Kocha wa kilabu cha Wazito FcC Boniface Ambani na wazaidizi wake Salim Babu na mkufunzi wa walinda lango Elias Otieno wamepigwa kalamu na usimamizi wa timu hiyo Jumatatu jioni bila sababu kutolewa.
Yamkini Ambani ambaye ni mchezaji wa zamani wa AFC Leopards hakufurahishwa na mambo yanavyoendeshwa kilabuni ikiwemo usajili wachezaji bila kuhusishwa.
Mfarakano kati ya Ambani ,wasaidizi wake wa ukufunzi na usimamizi wa timu ulionekana wazi wakati wa kipigo cha Wazito cha mabao 2-1 na Zoo Fc katika kaunti ya Kericho.

Ambani aliisaidia timu hiyo kupandishwa ngazi kucheza ligi kuu mwaka 2018 kabla ya kutimuliwa ambapo Melo Medis kutoka Misri alipokezwa jukumu hilo na kisha akatimuliwa huku pia wakufunzi Stanley Okumbi,Frank Ouna,Mwingereza Stewart Hall na kisha akarejea Ambani wote hao wakiwa wamefurushwa katika kipindi cha misimu miwili timu hiyo ikiwa katika ligi kuu.

Pia wazito timu hiyo imekuwa ikiwasajili na kuwatema wachezaji huku wakisajili wanandinga 15 na kuwapiga kalamu 14 katika uhamisho uliofungwa Novemba 6 mwaka huu.
Wazito FC iliwatimua makocha hao Jumatatu zikisalia akriban siku 10 kabla ya kuanza kwa msimu wa mwaka 2020/2021 wa ligi kuu.