“Wife Material itakuwa kubwa na bora zaidi” asema Eric Omondi

Mchekeshaji Eric Omondi amesema kwamba kipindi chake cha mitandaoni kwa jina Wife Material kitarejea kwa njia kubwa na bora. Usemi wake unafuatia mkutano uliofanyika kati yake na bodi ya kuorodhesha filamu nchini KFCB.

Baada ya mkutano huo wa jana, Eric na mkurugenzi mkuu wa KFCB Daktari Ezekiel Mutua walihutubia wanahabari ambapo walionekana kukubaliana kwamba vipindi vyote vinavyotayarishwa lazima viwe na kiwango fulani cha maadili.

Jana, Mutua alitangaza kwamba kipindi hicho kimesimamishwa kwa muda hadi pale ambapo kesi dhidi ya Eric Omondi itakapokamilika. Eric alisema wanakubali kwamba sio lazima kazi ya sanaa iwe chafu ili iuze.

KFCB iliamua kutatua suala la Eric kutayarisha kipindi bila idhini na bila kufuata masharti nje ya mahakama na mbele ya kamati ambayo inajumuisha wachekeshaji Daniel Ndambuki maarufu kama Churchill na Felix Odiwuor maarufu kama Mzee Jalang’o.

Na hii leo, Eric ameendelea kuelezea kuhusu yale ambayo waliafikiana kwenye mkutano wa jana kupitia akaunti yake ya Instagram ambapo amehakikishia wafuasi wake kwamba kipindi kitarejea.

Jambo lingine ambalo amezungumzia ni wasanii na watayarisha vipindi kujisimamia wenyewe na kwamba wasanii wataunda masharti ambayo wanadhani yanafaa kwa kuzingatia sheria zilizopo tayari.

Kulingana naye, huu ni ushindi kwa sekta nzima ya burudani kwani yeye ndiye wa kwanza na anatumai atakuwa wa mwisho kuwahi kukamatwa na polisi kwa ajili ya kuunda kazi ya sanaa.

Alifichua pia kwamba wiki hii, kamati maalum ya wasanii itaketi na kuandika masharti ambayo watatumia katika kujisimamia wanapoendesha kazi mbali mbali za sanaa.

  

Latest posts

Wasanii Wanaowakilisha Kenya AFRIMA

Marion Bosire

Akothee Apata Mgeni wa Heshima Kwenye Hafla Yake

Marion Bosire

KFCB Yazuia Usambazaji Wa Filamu

Marion Bosire

Tovuti hii inatumia kuki kukuhudumia vyema. Tafadhali kubali kupokea. Kubali Fahamu Zaidi